Mar 29, 2021 12:34 UTC
  • Maafisa Usalama Iraq wazima jaribio la shambulizi la kigaidi Karbala

Maafisa usalama wa Iraq wamezima jaribio la shambulizi la kigaidi lililolenga mjumuiko mkubwa wa wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) uliokuwa njiani kutoka Najaf ukielekea katika mji mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya sherehe za kuzaliwa Imam wa Zama na mwokozi aliyeahidiwa wa Akheri Zamani, Imam Mahdi (as).

Ripoti zinasema kuwa, gaidi mmoja wa kundi la Daesh jioni ya Jumapili ya jana, katika usiku wa kuamkia siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Imam wa Zama, Mahdi (as), alipanda gari la mazuwari lililokuwa likielekea Karbala kutoka Najaf na kujificha baina ya wapenzi wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) akiwa na shabaha ya kujilipua na kufanya mauaji ya kigaidi katika mji mtakatifu wa Karbala. 

Baada ya kutiwa nguvuni, gaidi huyo alijaribu kujifanya kiziwi na bubu lakini aliumbuka baada ya kufikishwa katika kituo cha usalama na kusailiwa.

Maeneo matakatifu ya Iraq yamekuwa chini ya ulinzi mkali tangu siku kadhaa zilizopita kwa hofu ya kutokea shambulizi la kigaidi dhidi ya Waislamu waliokua wakielekea katika maeneo hayo kuadhimisha siku ya kuzaliwa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Mahdi (as) ambaye hadithi zinasema, atakuja kuijaza dunia haki na uadilifu baada ya kujazwa dhulma na uonevu. 

Imam Mahdi (as) alizaliwa katika siku kama hii ya leo 15 Shaabani mwaka 255 Hijria huko Samarra nchini Iraq.  

Tags