Bahrain nayo yasema iko tayari kutuma askari Syria
Utawala wa Aal-Khalifa umesema Bahrain iko tayari kutuma askari wake wa nchi kavu nchini Syria, eti kupambana na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Hayo yamesemwa na Sheikh Fawaz Bin Muhammad Aal-Khalifa, Balozi wa Bahrain nchini Uingereza, muda mfupi baada ya Saudi Arabia kusema kuwa iko tayari kutuma vikosi vyake nchini Syria. Mwanadiplomasia huyo wa Bahrain amesema lengo la Saudia kutuma vikosi vyake nchini Syria ni kuwaangamiza magaidi wa Daesh sambamba na kuuangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Assad. Hii ni katika hali ambayo, Naibu Spika wa bunge la Russia ameitahadharisha Saudia kuhusu kupeleka wanajeshi wake nchini Syria na kusema kuwa, hatua kama hiyo itachukuliwa kama tangazo la vita endapo haitapata ridhaa ya serikali ya Damascus. Pavel Krasheninnikov amesema sheria za kimataifa zinazuia nchi yoyote kupeleka majeshi katika nchi nyingine bila ya ridhaa ya serikali husika. Kauli ya Saudi Arabia ya kupeleka wanajeshi katika ardhi ya Syria imetolewa baada ya magaidi wa Daesh kupata pigo kubwa kufuatia kuondolewa kwao na jeshi la Syria katika maeneo muhimu ya mkoa wa Halab (Aleppo) na kukatwa njia yao ya kusafirishia bidhaa kutoka Uturuki. Saudia ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa magaidi wa Daesh na makundi mengine ya kigaidi ndani ya Syria inataka kutuma majeshi yake ili badala ya kupambana na magaidi iweze kushambulia vikosi vya serikali na kurudisha mlingano katika vita vya Syria ambavyo kwa sasa vinaonekana kudhibitiwa na jeshi la serikali ya Damascus.