Khalid Mash'al achaguliwa kuwa kiongozi wa HAMAS nje ya Palestina
Duru zenye mfungamano na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema, Khalid Mash'al amechaguliwa kuwa kiongozi wa harakati hiyo nje ya Palestina.
Gazeti la Al-Qudsul Araby limeinukuu duru yenye mfungamano na Hamas ikiripoti kuwa, Mash'al, ambaye ni mkuu wa zamani wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo ya muqawama ya Palestina amechaguliwa kuwa kiongozi wa nje ya Palestina.
Afisa huyo wa Hamas ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia gazeti hilo kuwa, katika uchaguzi uliofanyika jana Jumatatu kwa madhumuni ya kumchagua kiongozi wa Hamas wa nje ya Palestina, Khalid Mash'al amechaguliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka minne.
Mash'al, alikuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kuanzia mwaka 1996 hadi 2017, wadhifa ambao kuanzia mwaka huo hadi sasa unashikiliwa na Ismail Haniya.
Mnamo tarehe 10 Machi mwaka huu, Hamas ilimchagua pia Yahya Sinwari kuwa kiongozi wa harakati hiyo ya mapambano ya ukombozi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Uchaguzi wa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas unatazamiwa kufanyika mwezi huu wa Aprili.../