HAMAS yatahadharisha kuhusu mpango wa kuakhirisha uchaguzi Palestina
(last modified Fri, 23 Apr 2021 02:23:59 GMT )
Apr 23, 2021 02:23 UTC
  • HAMAS yatahadharisha kuhusu mpango wa kuakhirisha uchaguzi Palestina

Afisa mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ameonya kuwa, hatua yoyote ya kubadilisha kalenda na ratiba ya uchaguzi wa Palestina ambao umesubiriwa kwa muda mrefu itatoa pigo kwa jitihada za kuzipatanisha tawala hasimu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Khalil al-Hayya, Mkuu wa kambi ya HAMAS katika uchaguzi wa mwezi ujao amesema azma ya kuakhirisha tarehe ya uchaguzi huo japo kwa siku chache itavuruga jitihada za kurejesha amani Palestina.

Amesema kubadilisha tarehe ya uchaguzi au kuakhirishwa kwa zoezi hilo si tu kutaibua migawanyiko miongoni mwa Wapalestina, lakini pia huenda kukawachochea vijana wakafanya mambo yasiyotabirika.

Al-Hayya amebainisha kuwa, HAMAS haipiganii sana kuongoza serikali ijayo ya Palestina, lakini inataka kuwa mshirika wa serikali ya umoja wa kitaifa.

HAMAS ilivyong'ara katika uchaguzi wa mwaka 2006

Afisa huyo mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameongeza kuwa, uchaguzi ujao wa Palestina ni fursa ya kuhitimisha migawanyiko na kuziunganisha taasisi za Wapalestina, mbali na kuhitimisha matatizo yao, na mzigiro wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Uchaguzi wa Bunge wa Palestina umepangwa kufanyika tarehe 22 mwezi ujao Mei mwaka huu, ule wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ukipngiwa tarehe 31 mwezi Julai huku ule wa Baraza la Taifa la Palestina ukitazamiwa kufanyika tarehe 31 Agosti mwaka huu. 

Tags