HAMAS: Tuna uwezo wa kuvurumisha mamia ya makombora kwa dakika
(last modified Thu, 27 May 2021 07:30:35 GMT )
May 27, 2021 07:30 UTC
  • HAMAS: Tuna uwezo wa kuvurumisha mamia ya makombora kwa dakika

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika Ukanda wa Gaza amesema harakati hiyo ya muqawama inayo uwezo wa kuvurumisha mamia ya makombora ndani ya dakika moja, yanayoweza kupiga umbali wa hadi kilomita 200, ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Yahya Sinwar alisema hayo jana Jumatano katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa: Muqawama uliodhihirishwa wakati wa kuihami Gaza, ni sehemu ndogo kabisa ya uwezo wa harakati hiyo.

Ameeleza bayana kuwa, taifa la Palestina kamwe halitaachana na muqawama na mapambano hadi lipate ushindi ambao utabadilisha muundo wote wa Mashariki ya Kati.

Israel ilianzisha vita dhidi ya raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na huko Gaza tangu tarehe 10 mwezi huu wa Mei; na kumalizika tarehe 21 kufuatia ombi la baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni na upatanishi wa baadhi ya pande ajinabi baada ya kushindwa jeshi la utawala huo kukabiliana na wanamuqawama wa Palestina.

Harakati za muqawama katika Ukanda wa Gaza zilijibu chokochoko hizo za Wazayuni kwa kuvurumisha maroketi na makombora 4000 kuelekea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.

Makombora ya HAMAS

Sinwar amebainisha kuwa: Wakati wa kuelekea kumalizika vita hivyo, HAMAS ilisitisha mpango wa Brigedi za Izzudin al-Qassam ambazo ni tawi la kijeshi la harakati hiyo ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, wa kukomesha uvamizi wa Tel Aviv kwa kuvurumisha makombora 300 kwa mpigo kuelekea Israel.

Kadhalika amepuuzilia mbali madai ya Wazayuni kwamba wamesambaratisha barabara za chini ya ardhi za harakati hiyo katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa: Tuna barabara za chini ya ardhi zenye urefu wa kilomita 500 katika Ukanda wa Gaza, na sehemu iliyoharibiwa ni asilimia 5 tu.

Tags