Wapalestina waandamana Siku ya Nakba, wasisitiza mapambano dhidi ya Israel
Wapalestina wameandamana Jumapili katika maeneo mbalimbali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 68 tangu ulipoundwa utawala bandia na haramu wa Israel mwaka 1948.
Maelfu ya Wapalestina wameandamana katika Ukanda wa Ghaza, wakitaka kurejea katika ardhi zao za asili zilizoporwa na Israel mwaka 1948.
Huku wakitoa nara ya 'Tutarudi', Wapalestina wamesema hawawezi kusahau ardhi zao ambazo ziliporwa wakati wa kuundwa dola bandia la Israel. Aidha wamesisitiza kuhusu umoja baina ya makundi ya Wapalestina huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ili kufanikisha mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel. Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni umekuwa ukijaribu bila mafanikio kuzuia kufanyika maandamano ya Wapalestina kukumbuka masaibu ya Siku ya Nakba.
Wakati huo huo kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Khalid Meshaal katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Nakba amesema, 'haki ya kurejea, kuachiliwa huru wafungwa, utaifa na kujitawala ni haki zisizo pingika za Wapalestina.
Wapalestina zaidi ya 750,000 walitimuliwa kutoka ardhi zao mwaka 1948 wakati wa kuundwa dola haramu la Israel na hivyo wakasambaratika katika kambi za wakimbizi huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi, Syria, Jordan, Lebanon na maeneo mengine duniani. Hivi sasa kunakadiriwa kuwepo wakimbizi zaidi ya milioni tano Wapalestina duniani.