"Chinjachinja" wa kundi la kigaidi la Daesh aangamizwa nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71538-chinjachinja_wa_kundi_la_kigaidi_la_daesh_aangamizwa_nchini_iraq
Harakati ya wananchi wa Iraq ya al Hashdul Shaabi imetangaza kuwa imefanikiwa kumuangamiza mmoja kati ya viongozi hatari zaidi wa kundi la kigaidi la Daesh ambaye alikuwa maarufu kwa jina la "Chinjachinja" katika mkoa wa Diyala.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 22, 2021 07:20 UTC

Harakati ya wananchi wa Iraq ya al Hashdul Shaabi imetangaza kuwa imefanikiwa kumuangamiza mmoja kati ya viongozi hatari zaidi wa kundi la kigaidi la Daesh ambaye alikuwa maarufu kwa jina la "Chinjachinja" katika mkoa wa Diyala.

Maafisa wa al Hashdul Shaabi wamesema kuwa, kinara huyo wa kundi la Daesh aliuawa katika operesheni ya kushtukiza iliyofanywa na wapiganaji wa harakati hiyo kandokando ya kitongoji cha al Miqdadiya kilichoko umbali wa kilomita 45 kaskazini mashariki mwa mji wa Baaquba.

Waafisa hao wamesema kuwa wapelelezi wa Divisheni ya 24 ya al Hashdul Shaabi wamefanikiwa kumuangamiza Usamah al Nahir, "chinjachinja" wa kundi la Daesh aliyekuwa miongoni mwa vinara hatari zaidi wa kundi hilo la kigaidi, baada ya miaka mingi ya kumuwinda na kumkosakosa gaidi huyo mkubwa. 

Wameongeza kuwa, kuangamizwa kwa al Nahir kumetimia kutokana na ripoti makini za kipepelezi na kwamba kuuawa kwake ni pigo kubwa kwa mabaki ya kundi hilo nchini Iraq hususan katika mkoa wa Diyala. 

Harakati ya wananchi wa Iraq ya al Hashul Shaabi inaendeleza operesheni ya kuwasaka mabaki ya kundi la kigaidi la Daesh ambalo linahuishwa na mauaji na ukatili wa kutisha katika nchi za Iraq na Syria miaka kadhaa ya karibuni.