Makumi ya wapiganaji wa ISIS wauawa katika mapigano na vikosi vya Puntland, Somalia
Makumi ya wanamgambo wa ISIS wameuawa katika makabiliano makali na vikosi vya usalama katika eneo linalojitawala la Puntland huko Somalia jana Jumatano, huku vikosi vya usalama vikipata hasara katika mapigano hayo yaliyoanza Jumanne iliyopita.
Maafisa wa kijeshi katika eneo la Puntland wamesema kuwa vikosi vya jeshi vimezuia mashambulizi ya kundi la Daesh kwenye moja ya kambi zake katika milima ya Alimiskaad.
Kamanda mmoja wa kijeshi amesema mapigano hayo yalianza wakati watu wawili waliokuwa na silaha waliposhambulia kambi ya jeshi wakiwa kwenye gari lililokuwa na mabomu, na kuongeza kuwa shambulio hilo lilizuiwa baada ya mapigano makali.
Kamanda huyo ameongeza kuwa, idadi kadhaa ya wanamgambo wa Daesh waliokuwa wamevalia fulana za vilipuzi walijilipua na kusababisha hasara katika safu za jeshi. Afisa mwingine wa pia amethibitisha kuwa zaidi ya wanajeshi 20 wa Puntland wameuawa katika mapigano hayo.
Ni vyema kutambua kwamba Desemba mwaka jana mamlaka ya Puntland ilianzisha mashambulizi dhidi ya kundi la Daesh (ISIS) katika eneo hilo.
Ingawa uwepo wa kundi hilo nchini Somalia ni mdogo ikilinganishwa na kundi la al-Shabaab lenye uhusiano na al-Qaeda, lakini shughuli zake zimeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni, na kiongozi wa ISIS nchini Somalia, Abdulqadir Mumin, anaaminika kuongoza operesheni kutoka eneo Puntland.