Muungano vamizi wa Saudia waua na kujeruhi raia 20 Yemen
(last modified Thu, 01 Jul 2021 10:51:45 GMT )
Jul 01, 2021 10:51 UTC
  • Muungano vamizi wa Saudia waua na kujeruhi raia 20 Yemen

Muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umeua na kujeruhiwa raia wapatao 20 katika hujuma dhidi ya mkoa wa Sa'ada nchini Yemen.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Masirah, Jumatano usiku muungano vamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia ulishambulia eneo la mpakani la Ar Raqo  mkoani Sa'ada kaskazini mwa Yemen ambapo kwa uchache raia wawili wameuawa na wengine sita kujeruhiwa.

Aidha katika hujuma nyingine muungano vamizi wa Saudia mapema leo umetekeleza hujuma dhidi ya mji wa Shada katika mkoa huo huo wa Sa'ada ambapo raia wengine wawili wamejeruhiwa.

Kwa ujumla raia 20 Wayemen wameuawa au kujeruhiwa katika hujuma mbali mbali za Saudi Arabia katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo.

Mtoto wa Yemen aliyejeruhiwa katika hujuma ya Saudia

Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, UAE na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani ambao unaendelea hadi sasa.

Vita hivyo vya Saudia vimesababisha maafa makubwa zaidi ya kibinadamu nchini Yemen.

Kwa mujibu  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA),  vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Idadi kubwa ya raia hasa wanawake na watoto ni waathirika wakuu wa hujuma za Saudia dhidi ya Yemen.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.