Hamas:Israel haiwezi kubadili mlingano
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, mashambulizi ya Wazayuni katika Ukanda wa Ghaza pia hayawezi kubadili mlingano.
Hizam Qassim leo ameeleza kuwa mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza ni hatua iliyofeli kwa ajili ya kusitisha jitihada za wananchi wa Palestina za kupigania haki zao. Msemaji wa Hamas ameongeza kuwa, wananchi wa Palestina na muqawama wao wataendeleza mapambano yao halali ili kupigania haki ya kuishi kwa uhuru na heshima. Msemaji wa Hamas amebainisha hayo katika radiamali yake kwa mashambulizi ya anga ya Israel huko Ghaza.
Duru za kieneo za Palestina leo asubuhi zimeripoti kujiri mashambulizi ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni katika maeneo ya kusini na kaskazini magharibi mwa Ukanda wa Ghaza.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Msemaji wa Hamas ametangaza habari ya kuchaguliwa Salah al Aruri kuwa Mkuu wa Ofisi ya harakati hiyo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Al Aruri ni mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa muqawama wa Palestina na Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa Kisiasa ya Hamas ambaye alikuwa na mchango mkubwa pia katika kuasisiwa brigedi za al Qassam ambayo ni matawi ya kijeshi ya harakati hiyo.