Iraq: Jamii ya Kimataifa ichukue msimamo kuhusu uvamizi wa Uturuki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Ibrahim al-Jaafari ameitaka Jamii ya Kimataifa ichukue msimamo unaojulikana kuhusiana na uvamizi uliofanywa na Uturuki dhidi ya ardhi ya nchi yake.
Al-Jaafari ameyasema hayo katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Philip Hammond pembeni ya kikao cha nchi zinazowasaidia wananchi wa Syria kilichofanyika mjini London.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesisitiza kuwa Mashariki ya Kati inashuhudia hali ya fadhaa na wasiwasi na kwamba unahitajika mchango mkubwa wa kidiplomasia ili kurejesha utulivu na uthabiti. Ameongeza kuwa sambamba na hayo, Iraq nayo inakabiliwa na matatizo kadhaa ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya ugaidi wa Daesh na kushuka kwa bei ya mafuta; hivyo katika mazingira hayo nchi rafiki zinapaswa kuisaidia nchi hiyo.
Akizungumzia uvamizi wa Uturuki katika ardhi ya Iraq, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Philip Hammond amesema Iraq inapita katika kipindi kigumu kinachohitajia msaada wa nchi zote; hata hivyo msaada huo utapasa kutolewa kwa ridhaa na makubaliano na serikali ya Baghdad.
Tangu majira ya joto mwaka jana, Iraq imekumbwa na mgogoro wa vita na mapigano baada ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kuvamia miji ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo.
Sambamba na hayo, mnamo tarehe 4 Disemba mwaka jana, makumi ya askari wa jeshi la Uturuki waliingia ndani ya ardhi ya Iraq katika eneo la Baashiqa mjini Mosul mkoani Nainawa huko kaskazini mwa nchi hiyo kwa kisingizio cha kwenda kutoa mafunzo kwa vikosi vya Kikurdi vya Peshmerga. Mbali na kusisitiza askari hao waondoke katika ardhi ya nchi hiyo, serikali ya Iraq imewasilisha malalamiko yake dhidi ya Uturuki katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.../