Haniya: Upanga wa Quds ulisambaratisha njama za kuuchafua muqawama
(last modified Mon, 23 Aug 2021 03:33:25 GMT )
Aug 23, 2021 03:33 UTC
  • Haniya: Upanga wa Quds ulisambaratisha njama za kuuchafua muqawama

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema vita vya Saif al Quds (Upanga wa Quds) vilizima njama na juhudi zote za kutaka kuipaka matope kambi ya muqawama.

Ismail Haniya amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Mehr na kuongeza kuwa, Operesheni ya Upanga wa Quds ilifungua ukurasa nyeti katika historia ya mapambano dhidi ya adui Mzayuni.

Amesema kuibuka na ushindi kambi ya muqawama katika vita hivyo vya siku 12, kulisambaratisha njama za maadui za kuuchafulia jina mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika eneo, licha ya mabilioni ya dola kutumika katika uwanja huo.

Haniya ameeleza bayana kuwa, vita vya Upanga wa Quds kwa mara nyingine tena viliweka wazi kuwa Quds ndicho kitovu kikuu cha mapambano ya wanamuqawama na maadui Wazayuni.

Wanamuqawama na zana zao za kivita

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amekumbusha kuwa, kadhia ya Palestina ni suala la umma wote wa Kiislamu, na kwamba muqawama ndilo chaguo la kistratajia la kumshinda adui, na wala si kupitia mazungumzo na kuutambua utawala wa Kizayuni. 

Vita vya Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ghaza vilianza tarehe 10 Mei mwaka huu na kumalizika tarehe 21 mwezi huo huo, baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kusalimu amri na kuomba kusitisha mapigano na wanamapambano wa Palestina.

 

Tags