Mahmoud Abbas 'amewapiga jambia' Wapalestina kwa kukutana na Gantz
Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS amesema kitendo cha Mamhoumd Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kukutana na kufanya mazungumzo na Benny Gantz, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel ni sawa na kuwachoma jambia kwa nyuma Wapalestina.
Abdul-Latif Al-Qanu amesema Mahmoud Abbas anaendelea kusaliti damu za mashahidi wa Kipalestina kwa mienendo yake hiyo. Msemaji huyo wa HAMAS ameeleza bayana kuwa, "kwa bahati mbaya, Mahmoud Abbas anaendelea kudunisha thamani za kitaifa za Wapalestina, kwa hatua zake za kujaribu 'kusafisha uso wa jinai wa Wazayuni."
Abbas hapo jana alikutana na Gantz katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu, huo ukiwa mkutano wa kwanza wa ngazi za juu wa pande mbili hizo, tangu serikali mpya ya Kizayuni iundwe mwezi Juni mwaka huu.
Kabla ya hapo, Fawzi Barhoum, msemaji wa HAMAS alisema Rais Mahmoud Abbas amekuwa akiipatia harakati ya muqawama masharti ambayo kimsingi ni yale yale ambayo yamekuwa yakitolewa na utawala haramu wa Israel.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, ushirikiano wa kiusalama wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Israel umeendelea kulalamikiwa na wananchi wa Palestina.
Wapalestina wanaaamini kuwa, taasisi za usalama za Mamlaka ya Ndani ya Palestina hazina jukumu jengine isipokuwa kukandamiza hatua yoyote ile ya kitaifa ya muqawama dhidi ya Wazayuni maghasibu, jambo ambalo linaupa fursa utawala wa Kizayuni ya kubomoa nyumba za Wapalestina, kujenga vitongoji vyengine zaidi na kufuta utambulisho wa Wapalestina.