"Kujipendekeza Abbas kwa Israel kunaashiria kudidimia Mamlaka ya Ndani Palestina"
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imekosoa vikali hatua ya Mamhoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kujidhalilisha na kuwaangukia miguuni maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, kitendo hicho kinaonesha namna mamlaka hiyo inavyoendelea kudidimia na kusambaratika.
Hazem Qassem, msemaji wa HAMAS katika Ukanda wa Gaza alisema hayo jana Jumatatu katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter na kueleza bayana kuwa, Abbas amejidhalilisha na kuudhalilisha uongozi wake, kwa kuomba kukutana na Waziri Mkuu wa Israel na Waziri wa Mambo ya Ndani mwenye misimamo ya kuchupa mipaka wa utawala huo khabithi.
Qassem amesema kujikomba na kujidhalilisha huko kunaonesha namna hulka na mienendo ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na uongozi wake inavyozidi kuporomoka.
Msemaji wa HAMAS katika Ukanda wa Gaza ameongeza kuwa, mienendo hii ya Abbas haijazaa kitu kingine ghairi ya kuushajiisha utawala haramu wa Israel kuendelea kulihujumu taifa la Palestina.
Usiku wa kuamkia jana Jumatatu, Abbas alikutana kwa siri na Nitzan Horowitz, Waziri wa Afya wa utawala wa Kizayuni na mwenzake wa Ushirikiano wa Kieneo, Esawi Freij mjini Ramallah, katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Aidha Agosti mwaka huu, Abbas alikutana na kufanya mazungumzo na Benny Gantz, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, huku HAMAS ikisisitiza kuwa kitendo hicho ni sawa na kuwachoma jambia kwa nyuma Wapalestina.
Abbas anaendelea kujikomba kwa Wazayuni katika hali ambayo, Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala khabithi wa Israel mwenye misimamo ya kufurutu ada amesisitiza mara kadhaa kuwa, kamwe hatoruhusu kuundwa dola la Palestina katika utawala wake.