HAMAS yakosoa hatua ya Saudia ya kuusifu utawala haramu wa Israel
Moussa Abu Marzouk, mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amekosoa vikali matamshi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia na kueleza kwamba, hakuna wakati wowote ule ambao Israel ilikuwa sababu ya amani na uthabiti Asia Magharibi na wala hakuna wakati itakuwa hivyo.
Faisal bin Farhan Al Saud, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia alidai hivi karibuni baada ya kukutana na Antony Blinken, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwamba, Israel imesaidia juhudi za kuleta amani na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.
Akijibu madai haya yasiyo na ukweli wowote, Moussa Abu Marzouk, mjumbe mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, tangu utawala haramu wa Israel ulipoasisiwa hadi leo kila mahala palipo na mizozo basi kuna mkono wa utawala huo ghasibu.
Kiongozi huyo wa Hamas amesema kuwa, mifano ya wazi ni Palestina, kusini mwa Lebanon, Misri, Sudan na mzozo wa Bwawa la al-Nahdha; hivyo ni kichekesho kusema kuwa, Israel imekuwa na mchango katika juhudi za kuleta amani na uthabiti.
Matamshi hayo ya Saudia ya kuusifu utawala ghasibu wa Israel yanatolewa katika hali ambayo, katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, haki za Wapalestina zimeporwa, nyumba zao zimebomolewa, ardhi zao kughusubiwa na kubwa zaidi katika kipindi hiki Israel imetenda jinai za kila aina dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Aidha Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa, hatua za jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina ni mfano wa wazi wa jinai za kivita.