Umoja wa Mataifa dhidi ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i76822-umoja_wa_mataifa_dhidi_ya_yemen
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewaweka viongozi watatu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na baraza hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 12, 2021 07:10 UTC
  • Umoja wa Mataifa dhidi ya Yemen

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewaweka viongozi watatu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na baraza hilo.

Ni miezi 80 sasa ambapo Yemen inashuhudia mashambulizi ya kila siku ya ndege za kivita za Saudi Arabia  na jinai zingine chungu nzima zinazotekelezwa na mamluki wa Saudia dhidi ya watu wa nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu.

Umoja wa Mataifa umewahi kutangaza bayana mara kadhaa kuwa, hivi sasa Yemen inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu kutokana na vita hivyo.  Karibu raia milioni nne wa Yemen wamelazimka kuwa wakimbizi kutokana na vita hivyo. Aidha zaidi ya watu laki moja wamepoteza maisha kutokana na vita hivyo vilivyoanzishwa na Saudia. Hali kadhalika malaki ya Wayemen pia wamejeruhiwa kutokana na mabomu yanayodondoshwa kila siku na Saudia katika nchi hiyo. Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa aliwahi kukiri kuwa, Saudi Arabia ni mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za watoto nchini Yemen.

Kwa mujibu wa hati ya kuanzishwa Umoja wa Mataifa, umoja huo unabeba jukumu la kulinda na kudumisha amani na usalama duniani. Hii ni taasisi muhimu zaidi ambayo kwa maamuzi yake ingeweza kupunguza maafa ya kibinadamu nchini Yemen. Hata hivyo katika mgogoro wa Yemen, taasisi hii imepoteza msingi wake muhimu ambao ni kutopendelea upande wowote katika migogoro ya kimataifa. Hivi sasa Umoja wa Mataifa umegeuka na kuwa muitifaki wa utawala wa Saudi Arabia katika vita vyake dhidi ya Yemen. Muelekeo huu wa Umoja wa Mataifa umepelekea mtazamo wa "kisiasa' kupata nguvu kuliko mtazamo wa "kisheria" katika mgogoro wa Yemen.

Wapiganaji wa Ansarullah nchini Yemen wakisherehekea ushindi

Katika hatua yake ya hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo Novemba 10 2021 lilitangaza kuwaweka viongozi watatu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen katika orodha yake ya watu waliowekewa vikwazo. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa, Abdulkarim al Ghamri, Yusuf al Madani na Saleh Musafir Saleh ndio waliowekwa katika orodha hiyo ya vikwazo ambayo pia ina wanachama wengine 9 wa Ansarulllah.

Nukta muhimu hapa ni hii kuwa, watu hao wote watatu waliowekwa katika orodha ya vikwazo ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Yemen ni katika maafisa waandamizi wa kijeshi wa Ansarullah na wamekuwa na nafasi kubwa katika mafanikio ya Jeshi la Serikali ya Uwokovu wa Kitaifa dhidi ya jeshi vamizi la Saudia na mamluki wake hasa katika mkoa wa Ma'rib.

Kamati ya vikwazo ya Umoja wa Mataifa imetoa taarifa na kusema watatu hao walikuwa na 'nafasi ya kistratijia katika oparesheni za kijeshi za Mahouthi' na kwamba eti walikuwa tishio kwa usalama, amani na uthabiti Yemen.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Abdulkarim al Ghanim alkuwa na nafasi muhimu katika kuratibu oparesheni za kijeshi za Ansarallah hivi karibuni katika mkoa wa Ma'rib. Yusuf al Madani naye ni kati ya viongozi wa Ansarallah alikyekuwa na jukumu la kusimamia kamandi ya vikosi vya harakati hiyo. Saleh al-Musafir Saleh ni mshauri wa Waziri wa Ulinzi wa Yemen katika masuala ya kilojistiki.

Watoto wa Yemen ni waathirika wakubwa wa vita vya Saudia dhidi ya nchi yao

Hatua hii ya Baraza la Usalama ni msaada wa wazi kwa muungano vamizi wa Saudia katika vita dhidi ya Yemen. Jeshi la Serikali ya Uwokovu wa Kitaifa ya Yemen katika miezi ya hivi karibuni limepata mafanikio makubwa katika vita huko Ma'rib na sasa mkoa huo unakaribia kukombolewa kikamilifu kutoka makucha ya mamluki wa Saudia. Kadhia hii imeutia hofu kubwa utawala wa Saudia  ambao sasa umetumia Baraza la Usalama kuwawekea vikwazo makamanda wa Ansarullah. Kwa msingi huo Baraza la Usalama limetangaza "kufungamana kisiasa" na utawala wa Saudia. Hakuna shaka kuwa hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa  haitakuwa na natija nyingine ghairi ya kuufanya kuwa mbaya zaidi mgogoro wa Yemen sambamba na kuupa utawala wa Saudia kiburi zaidi cha kuendeleza jinai zake dhidi ya watu wa Yemen.