Sababu za mamluki wa Saudia na Imarati kuondoka magharibi mwa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i76986-sababu_za_mamluki_wa_saudia_na_imarati_kuondoka_magharibi_mwa_yemen
Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa vikosi vya muungano vamizi wa Saudi Arabi-Imarati vikiondoka katika ngome zao katika mji wa bandari wa al-Hudaydah.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 16, 2021 22:59 UTC
  • Sababu za mamluki wa Saudia na Imarati kuondoka magharibi mwa Yemen

Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa vikosi vya muungano vamizi wa Saudi Arabi-Imarati vikiondoka katika ngome zao katika mji wa bandari wa al-Hudaydah.

Alkhamisi iliyopita iliripotiwa kuwa, askari mamluki wa muungano wa Saudia na Imarati walichukua hatua ya ghafla ya kuondoka katika makumi ya ngome zao kusini na mashariki mwa mkoa wa al-Hudaydah uliopo magharibi mwa Yemen.

Baada ya mamluki hao wanaoungwa mkono na Imarati kukimbia na kuziacha ngome zao hizo, jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na kamati za ukombozi za kujitolea za wananchi haraka zilikwenda na kuyadhibiti maeneo hayo. Serikali iliyojiuzulu ya Rais Abdurabbuh Mansur Hadi aliyeikimbia nchi, imetangaza kuwa, haukushirikishwa wala kufahamishwa kuhusiana na hatua ya vikosi hivyo ya kurejea nyuma na kuondoka katika ngome zake. Hata Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ambao unaunga mkono makubaliano ya al-Hudaydah umetangaza kuwa, haukuwa na taarifa yoyote kuhusiana na kuondoka askari wa muungano huo kutoka katika ngome na maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti.

Swali linaloulizwa na wajuzi na weledi wa mambo ni kuwa, sababu hasa ya kuondoka ghafla na kusikotarajiwa vikosi vya muungano wa Saudi Arabia na Imarati katika maeneo yake ni nini hasa?

 

Kuna sababu kadhaa zinazotajwa na wajuzi wa mambo kuhusiana na hatua hiyo. Sababu ya kwanza ni kuwa, matukio ya Ma'rib huenda ikawa sababu ya askari wa muungano huo kuondoka huko al-Hudaydah. Katika siku za hivi karibuni, jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na kamati za ukombozi za kujitolea za wananchi limepata mafanikio makubwa huko Ma'rib na kukaribia kuukomboa mji huo kikamilifu.

Kuhusiana na hilo, duru za Yemen zimetangaza kuwa, askari wa muungano vamizi wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wamechukua uamuzi wa ghafla wa kuondoka katika maeneo yao ya kusini na mashariki mwa mkoa wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen katika kile ambacho kinahesabiwa ni kujaribu kwenda kuwasaidia wapiganaji wa Abdurabbuh Mansour Hadi mkoani Ma'rib. Uwezekano wa kuelekea Ma'rib wavamizi hao umepata nguvu baada ya askari hao wa muungano vamizi kuelekea upande wa mji wa al-Makha (Mocha) wa magharibi mwa mkoa wa Taiz.

Mamluki wa Saudia nchini Yemen

 

Sababu nyingine ya kuondoka askari wa muungano vamizi wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) huko Yemen inarejea katika wasiwasi Imarati wa hatua tarajiwa za jeshi la Yemen na kamati za ukombozi za kujitolea za wananchi dhidi ya Abu Dhabi. Salim al-Muntasir, mweledi na mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Yemen ameashiria indhari ya Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa Majeshi ya Yemen.

Brigedia Jenerali Saree alisema kuwa, kama Imarati itaendelea na hujuma na uvamizi wake dhidi ya Yemen, kutatekelezwa operesheni ya kijeshi muda si mrefu dhidi ya nchi hiyo hususan katika miji ya Dubai na Abu Dhabi na makumi ya maeneo ya nchi hiyo yatalengwa kwa mashambulio. Salim al-Muntasir ameashiria tishio hilo na kusema kuwa, Imarati kwa kutambua kwamba, Brigedia Jenerali Yahya Saree hana mzaha na jambo hilo, imechukua hatua hiyo ili kuepusha uwezekano wa kuandamwa kwa mashambulio na ndio maaana imetoa amri ya vikosi vyake kuondoka katika ngome na maeneo viliyokuwa vikiyadhibiti ili kupunguza hasira za Wayameni.

Sababu nyingine inayotajwa kuhusiana na kuondoka askari askari hao huko al-Hudaydah ni kuwa, Riyadh na Abu Dhabi kwa kuondoka katika mji wa bandari wa al-Hudaydah zinafanya juhudi za kulikinaisha jeshi la Yemen na kamati za ukombozi za kujitolea za wananchi ili zisizonge mbele katika kutekeleza mkakati wao wa kuukomboa mji wa Ma'rib, jambo ambalo bila shaka haliwezi kukubaliwa katu na Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen.

Mansur Hadi Rais wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia

 

Tukiachana na suala la kutaka kujua ni sababu gani hasa iliyowafanya au zilizowafanya mamluki wa Saudi Arabia na Imarati kuondoka katika pwani ya magharibi mwa Yemen, ukweli wa mambo ni kwamba, hatua hiyo inaonyesha kuwa, serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi imepoteza kabisa itibari yake, kwani uamuzi huo umechukuliwa  pasi na kushirikishwa wala kufahamishwa.

Feisal al-Hudhaifi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha al-Hudayydah katika kitivo cha Sayansi ya Siasa ameiambia Kanai ya Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kwamba: Kuondoka mamluki wanaoungwa mkono na Imarati huko al-Hudaydah kumefanyika katika fremu ya kudhamini maslahi ya waungaji mkono wa vikosi hivyo yaani Imarati na kupuuza maslahi ya serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi.