Haniya: Iran ni nguzo muhimu ya kambi ya muqawama
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuitaja kama nguzo kuu na muhimu ya mrengo wa muqawama wa Wapalestina.
Ismail Haniya amesema hayo katika mahojiano yaliyorushwa hewani jana usiku na televisheni ya al-Aqsa inayotangaza kwa lugha ya Kiarabu na kuongeza kuwa, "Uhusiano wetu na Iran ni wa kistratajia kwa kuwa Iran ni moja ya nguzo kuu za kambi ya mapambano."
Haniya ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kama roho ya kambi ya muqawama, imeufanyia mengi kwa maneno na vitendo mrengo huo.
Amefafanua kwa kusema kuwa, si siri kwamba Iran inaipa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) msaada ya kisiasa, kifedha, kijeshi na kiteknolojia.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS ameikosoa vikali Saudi Arabia na sera zake dhidi ya muqawama, haswa hatua ya utawala huo wa kifalme ya kuwafunga jela wanachama wa harakati hiyo ya mapambano nchini Saudia.
Haniya amebainisha kuwa, hukumu dhidi ya wanachama wa HAMAS haina tafsiri nyingine isipokuwa ni hukumu dhidi ya wananchi wote wa Palestina.