Palestina: Baraza jipya la mawaziri la Israel tishio kwa eneo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i7804-palestina_baraza_jipya_la_mawaziri_la_israel_tishio_kwa_eneo
Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, baraza jipya la mawaziri la utawala haramu wa Israel ni tishio kwa usalama na utulivu wa eneo zima la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 25, 2016 09:56 UTC
  • Palestina: Baraza jipya la mawaziri la Israel tishio kwa eneo

Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, baraza jipya la mawaziri la utawala haramu wa Israel ni tishio kwa usalama na utulivu wa eneo zima la Mashariki ya Kati.

Saeb Erakat amesema hatua ya Israel ya kumteua Avigdor Lieberman kuwa Waziri wa Vita wa utawala huo wa Kizayuni licha ya kuwa na misimamo misimamo mikali ya kufurutu ada, ni kuhatarisha usalama na amani ya eneo hili zima.

Amesema uteuzi wa Lieberman mwenye misimamo ya mrengo wa kulia utafungua mlango wa kuongezeka misimamo mikali, ubaguzi na udini.

Wakati huo huo, Sami Abu Zuhri, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, tawi la Ukanda wa Ghaza amekosoa kuteuliwa Lieberman kuwa Waziri wa Vita wa utawala katili wa Israel na kusema kuwa hatua hiyo itashadidisha machafuko katika eneo hili.

Hata hivyo Hamas imesema mwito wa Lieberman wa kutaka kuuawa makamanda waandamizi wa harakati hiyo ya Palestina ni vitisho visivyowababaisha.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Vita, Lieberman ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala haramu wa Israel aliwahi kulitaka jeshi la utawala huo pandikizi kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Wapalestina na pia kufanya juu chini kumuua Ismail Haniya, kiongozi mwandamizi wa Hamas.

Aidha aliwahi kudai kuwa, kuuawa Khalid Masha'al, kiongozi mwingine mwandamizi wa HAMAS ndiyo njia pekee ya kukomesha ujenzi ya barabara za chini ya ardhi za Hamas katika Ukanda wa Ghaza.