Utawala wa Israel wabomoa kituo cha afya cha Wapalestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel umebomoa kituo cha afya na majengo mengine kadhaa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo.
Duru za habari Palestina zinadokeza kuwa, askari wa utawala wa Israel wakiwa katika magari ya deraya walivamia kijiji cha Jabel al Mukaber kusini mashariki mwa Quds ambapo walisimamia mabuldoza ambayo yalibomoa Kituo cha Afya cha Abdullah al Sheikh.
Aidha mabuldoza hayo ya utawala wa Israel yalibomoa jengo jingine katika eneo la Beit Hanina kaskazini mwa mji wa Quds.
Halikadhalika Jumanne magari ya jeshi la Israel yalivamia kijiji cha Al Zaeem mashariki mwa mji wa Quds na kuharibu mashamba ya Wapalestina.
Utawala dhalimu wa Israel mara kwa mara hubomoa nyumba za Wapalestina kwa visingizio mbali mbali kwa lengo la kuwapa makazi haramu walowezi wa Kizayuni.
Utawala haramu wa Israel ulikalia kwa mabavu ardhi za magharibi mwa mji mtakatifu wa Quds ambazo zinajumuisha Msikiti wa al-Aqsa ambao ni msikiti wa tatu kwa utukufu katika ulimwengu wa Kiislamu mwaka 1948. Mwaka 1967 ulikalia kimabavu ardhi zaidi za mashariki ambazo Mamlaka ya Ndani ya Palestina imedhamiria kuzifanya kuwa mji mkuu wake.
Licha ya kuwa jamii ya kimataifa inazichukulia ardhi hizo kuwa zinakaliwa kwa mabavu na utawala wa kibaguzi wa Israel lakini haijachukua hatua zozote za maana za kuulazimisha utawala huo uwarudishie Wapalestina ardhi zao hizo.
Desemba 23, 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.