Wanajeshi wa Kizayuni waendelea kubomoa nyumba za Wapalestina
(last modified Wed, 12 Jan 2022 15:46:03 GMT )
Jan 12, 2022 15:46 UTC
  • Wanajeshi wa Kizayuni waendelea kubomoa nyumba za Wapalestina

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamebomoa nyumba 11 za raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel leo Jumatano wamebomoa nyumba 11 , kituo cha huduma mbali mbali na kisima cha maji ya Wapalestina katika eneo la Al Fakhiyat mashariki mwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Yatta kusini mwa eneo la Al Khalil.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, katika mwaka uliopita wa 2021, utawala wa Kizayuni ulibomoa nyumba 862 za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Mashariki.

Juzi pia makumi ya walowezi wa Kizayuni waliuvamia tena msikiti wa al-Aqsa huko Palestina na kuuvunjia heshima msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Ripoti ya Palestina al-Yaum inaeleza kuwa, katika muendelezo wa hujuma na vitendo vya chuki vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, makumi ya walowezi wa Kiyahudi jana walivamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqsa.

Mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel

Kwa muda mrefu sasa utawala wa Kizayuni umekuwa ukipora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa lengo la kuvuruga muundo wa kijiografia na kijamii katika maeneo ya Wapalestina kwa uungaji mkono wa kila upande wa Marekani.

Utawala wa Kizayuni unaendeleza ujenzi huo haramu wa vitongoji katika ardhi za Palestina huku ukipuuza takwa la jamii ya kimataifa la kusimamisha ujenzi huo. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ujenzi wa vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ni kinyume cha sheria.  

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hadi sasa utawala wa Israel haujachukua hatua yoyote ya kutekeleza azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

Tags