Jinai za Saudia nchini Yemen, malengo, radiamali na matokeo yake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i79536-jinai_za_saudia_nchini_yemen_malengo_radiamali_na_matokeo_yake
Utawala wa kiimla wa Saudi Arabia unaendelea na jinai zake katika nchi ya Waislamu ya Yemen ambapo katika matukio ya hivi karibuni, madola vamizi yakiongozwa na Saudia yameua kwa umati raia wasiopungua 77 wasio na hatia wa Yemen na kujeruhi wengine wapatao 230.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2022 23:08 UTC
  • Jinai za Saudia nchini Yemen, malengo, radiamali na matokeo yake

Utawala wa kiimla wa Saudi Arabia unaendelea na jinai zake katika nchi ya Waislamu ya Yemen ambapo katika matukio ya hivi karibuni, madola vamizi yakiongozwa na Saudia yameua kwa umati raia wasiopungua 77 wasio na hatia wa Yemen na kujeruhi wengine wapatao 230.

Mwaka huu wa 2022 umeanza na ongezeko la jinai za wavamizi wa Yemen hasa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa kawaida wasio na ulinzi wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Mwaka huu umeanza huku wanamapambano wa Yemen nao wakizidi kuonesha nguvu zao katika medani za mapambano kiasi kwamba mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, wanamapambano hao walifanikiwa kuisimamisha na kuikamata meli ya Imarati iliyokuwa imesheheni silaha za kivita zilizokuwa zinapelekwa kwenda kuua raia wa Yemen. Kukamatwa meli hiyo lilikuwa pigo kubwa kwa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia. 

Kabla ya hapo pia, Wayemen walikuwa wakiuonya Umoja wa Falme za Kiarabu uache kushiriki katika jinai na vita visivyoihusu nchi hiyo huko Yemen. Aidha waliwaonya viongozi wa Abu Dhabi kuwa majibu ya Wayemen kwa jinai zinazofanywa na Imarati yatakuwa makali, hata hivyo viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu walidharau maonyo hayo. Sasa ili kuonesha kwamba walikuwa hawatanii, Wayemen walifanya opereshenei kali waliyoipa jina la Tufani ya Wayemen na walipiga kwa makombora eneo la viwanda na uwanja wa ndege wa Abu Dhabi nchini Imarati na kusababisha hasara na woga mkubwa kwa viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Amma jambo la kuchekesha na pia kukirihisha ni kwamba, viongozi wa Saudia na Imarati, licha ya kwamba wanafanya jinai za kila siku dhidi ya wananchi wa Yemen kwa miaka mingi sasa, lakini wanataka Wayemen wakae kimya bila ya kutoa majibu yoyote dhidi yao na pale Wayemen hao wanapoendesha operesheni za kulipiza kisasi, viongozi wa nchi vamizi za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu wanakuwa wakali sana, wanalalamika dunia nzima na wanajifanya wameonewa. Si hayo tu, lakini pia wanaamua kumalizia hamaki zao kwa wananchi wa kawaida kama walivyofanya kwenye jinai yao ya siku ya tarehe 21 mwezi huu wa Januari wakati waliposhambulia jela moja huko Saada, kaskazini mwa Yemen na kuua kwa umati raia 77 wa kawaida na kujeruhi wengine 230.

Jinai kubwa ya Wasaudia na Waimarati ndani ya msikiti nchini Yemen

 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, katika jinai yao hiyo mpya, Wasaudia na Waimarati walikuwa na malengo mawili makuu.

Kwanza ni kumalizia hamaki zao kwa wananchi wa kawaida baada ya Wayemen kufanya operesheni ya kulipiza kisasi waliyoipa jina la Tufani ya Wayemen huko Abu Dhabi, Imarati. Kwa kweli lengo la Riyadh katika jinai yake hiyo ni kuonesha kuwa, bado iko pamoja na mvamizi mwenzake Imarati katika kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Yemen na kwa namna fulani kuuchochea Umoja wa Falme za Kiarabu ushiriki zaidi katika vita vya Yemen.

Pili Saudia imefanya jinai hiyo mpya kwa lengo la kuwatia hofu Wayemen na kuwaonesha kuwa, kama wataendelea kufanya mashambulio ya kulipiza kisasi dhidi ya Saudia na Imarati, basi wao watakuwa wanashambulia makazi ya watu na kuua kwa umati raia wa kawaida. Hilo limethibitishwa na Muhammad al Bukhaiti, mjumbe mwandamizi wa Baraza la Kisiasa la Ansarullah aliposisitiza kuwa, lengo la jinai za hivi karibuni za muungano vamizi wa Saudia-Imarati ni kutia hofu katika nyoyo za wananchi wa Yemen.

Amma cha kusikitisha ni kuona kuwa, mauaji ya umati yaliyofanywa na Saudia ya kuua raia 77 kwa mpigo na kujeruhi wengine 230 huko Yemen, yamedharauliwa na taasisi za kimataifa kana kwamba hakuna binadamu yoyote aliyeuawa. Wakati ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa kauli kali ya kulaani operesheni ya kulipiza kisasi iliyofanywa hivi karibuni na Wayemen, huko Imarati.

Jinai za Saudia na Imarati zinafanyika dhidi ya watoto wadogo na raia wa kawaida wa Yemen mbele ya kimya cha kutisha cha jamii ya kimataifa

 

Antony Blinken, waziri wa mambo ya nje wa Marekani hata hakugusia kabisa jinai za Saudia na Imarati nchini Yemen ambazo zinafanyika kwa silaha za madola ya Magharibi, bali ametosha tu na kusema wanazitaka pande zinazopigana Yemen kutatua masuala yao kidiplomasia. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres naye hakulaani jinai za Saudia bali ameishia kusema tu kuwa, kushambulia raia na miundombinu ya kiraia kunakinzana na sheria za kimataifa. Tab'ani Guterres ametaka kufanyike uchunguzi kuhusu jinai hizo mpya za Saudi Arabia nchini Yemen na kuwajibishwa wahusika.

Wayemen wamesema wazi kwamba matamshi kama hayo ya kiwogawoga ya Umoja wa Mataifa ambayo hayana athari zozote katika vitendo, hayawezi kuwapunguzia machungu wanayobebeshwa na wavamizi wa nchi yao. Lakini pia wanasisitiza kuwa, madola vamizi hata yakifanya jinai kubwa kiasi gani, hayawezi kulipigisha magoti taifa la mashujaa la Yemen.

Wachambuzi wa mambo wanasema, kuna uwezekano wa kuongezeka mapigano baina ya Wayemen na Wasaudia na Waimarati hasa baada ya Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree kuyaonya mashirika ya kigeni yaondoke nchini Imarati ili mashambulio ya kulipiza kisasi ya Wayemen yasije yakayasababishia hasara za mali mashirika hayo.