Mashinikizo yailazimisha US kusimamisha kuizuia Saudia mabomu ya vishada
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i7960-mashinikizo_yailazimisha_us_kusimamisha_kuizuia_saudia_mabomu_ya_vishada
Kufuatia mashinikizo ya jamii ya kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, Marekani imesimamisha kwa muda muamala wa kibiashara wa kuiuzia Saudi Arabia mabomu ya vishada.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2016 02:21 UTC
  • Mashinikizo yailazimisha US kusimamisha kuizuia Saudia mabomu ya vishada

Kufuatia mashinikizo ya jamii ya kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, Marekani imesimamisha kwa muda muamala wa kibiashara wa kuiuzia Saudi Arabia mabomu ya vishada.

Afisa mwandamizi wa serikali ya Washington ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameliambia jarida la Foreign Policy linalochapisha masuala ya sera za nje za Marekani kuwa, kufuatia ukosoaji wa Bunge la Kongresi la nchi hiyo na baada ya kubainika kuwa utawala wa Aal-Saud unatumia mabomu ya vishada dhidi ya maeneo ya raia nchini Yemen, serikali ya Washington imesitisha kwa muda kuiuzia Riyadh mabomu hayo.

Hatua hiyo ya Marekani inajiri siku chache baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kuikosoa Marekani kwa kuiuzia Saudi Arabia mabomu ya vishada yanayotumiwa na utawala huo wa kifalme dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen. Hadi sasa watu wasiopungua 9,400 wameshauawa na wengine zaidi ya 16,000 wamejeruhiwa tangu Saudia na washirika wake walipoanzisha mashambulio na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka jana kwa lengo la eti kumrejesha madarakani kibaraka wa utawala wa Aal Saud, Rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi. Mashambulio hayo yameangamiza na kusababisha hasara kubwa kwa miundombinu ya Yemen, mbali na kulenga na kubomoa hospitali, shule, misikiti na turathi za kihistoria za nchi hiyo.