Marekani na Isreal; wachezaji wanaonufaika zaidi na vita vya Yemen
Akizungumza siku ya Jumanne katika kikao na jumbe mbili za makabila ya eneo la al-Jauf na Maarib ya nchini Yemen, Abdulmalik al-Huthi, Kiongozi cha harakati ya Ansarullah amesema Wamarekai na Waisraeli ni maadui wakuu wa Waislamu na kwamba wanajaribu kunufaika na matatizo yaliyoko katika Umma wa Kiislamu ili kufikia malengo yao haramu katika eneo.
Mwaka wa saba wa vita vya kivamizi vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia huko Yemen unaelekea kumalizika. Vita hivyo visivyo vya uwiano vinavyoongozwa na nchi mbili tajiri zaidi za Kiarabu, yaani Saudi Arabia na Imarati dhidi ya nchi masikini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu, Yemen, vimeibua maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika karne ya 21.
Licha ya kuwa Marekani na utawala haramu wa Israel hazishiriki moja kwa moja katika vita hivyo lakini ni wazi kuwa ndizo zinazonufaika pakubwa na vita hivyo vya kinyama dhidi ya taifa lisilo na hatia.
Marekani inaziunga mkono kisiasa na kisilaha Saudi Arabia na Imarati dhidi ya Yemen. Silaha hizo ndizo zinaunda sehemu kubwa ya silaha zinazotumika dhidi ya watu wa Yemen. Wakati huo huo Marekani inatumia vibaya nafasi yake katika taasisi na mashirika ya kimataifa na hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia kupitishwa maazimio na uamuzi wowote wa kimataifa dhidi ya tawala za Riyadh na Abu Dhabi. Akiwa katika kampeni zake za uchaguzi na hata baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Marekani, Rais Joe Biden alikiri kwamba nchi yake ilikuwa ikitoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Saudia na Imarati katika vita vya Yemen na kuahidi kusimamisha msaada huo lakini hadi sasa hajachukua hatua yoyote ya kutekeleza ahadi yake hiyo.
Tovuti ya jarida la New Republic katika toleo lake la mwezi Januari mwaka huu liliandika kwamba: Licha ya ahadi zilizotolewa na Rais Joe Biden za kumaliza vita vya Yemen lakini bado mauzo ya silaha za Marekani kwa Saudia na Imarati yangali yanaendelea na Saudia inatumia silaha hizo kuendeleza masaibu na maafa nchini Yemen. Ukweli wa mambo ni kuwa uungaji mkono huo wa Marekani kwa Saudia na Imarati ni moja ya sababu zinazowapelekea Wasaudi na Waimarati kupata kiburi cha kuendeleza vita na jinai katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu
Utawala haramu wa Israel pia una nafasi muhimu katika vita hivyo. Katika toleo lake la mwezi Disemba mwaka uliopita, gazeti la Washington Post liliandika kwamba: Israel ni mshirika mkubwa katika vita dhidi ya Yemen. Utawala huo unashiriki katika vita hivyo kwa kuzipa Saudia na Imarati zaidi ya marubani 42 wa ndege za kivita na karibu wataalamu wa kijeshi na kiufundi 70. Kabla ya hapo gazeti la Kizayuni la Haaretz pia lilisisitiza kuwa shirika moja la Israel linalomilikiwa na viongozi wa utawala huo lilikuwa likitoa mafunzo ya kijeshi kwa vibaraka wa Saudia nchini Yemen.
Mbali na hayo Marekani na utawala huo haramu ndizo zinanufaika zaidi na vita vinavyoendelea huko Yemen. Kwa upande mmoja vita hivyo vinaziletea faida kubwa ya kifedha na kiuchumi kwa sababu kwa njia hiyo zinaziuzia silaha nchi tajiri za Kiarabu na kwa upande wa pili kuendelea vita hivyo kuna maana ya kuendelea tofauti na mifarakano ya nchi za Kiislamu. Jambo hilo bila shaka linakidhi matakwa na malengo ya Marekani na utawala wa kigaidi wa srael katika eneo la Asia Magharibi. Katika uwanja huo, Sayyid Abdulmalik al-Huthi, kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza kwamba Wamarekani na Waisraeli ndio maadui wakuu wa Waislamu na hasa taifa la Yemen na kwamba wanatumia mbinu tofauti kwa ajili ya kueneza chuki na kuwatenganisha Waislamu ili wafikie lengo lao la mwisho ambalo ni kujinufaisha kisiasa na kiuchumi na wakati huohuo kuchochea matatizo ya ndani ya ulimwengu wa Kislamu na Kiarabu.