Bin Salman aanzisha mradi wa ujasusi akishirikiana na Israel
Duru za habari zimetangaza kuwa, utawala wa Saudi Arabia meanzisha mradi mkubwa zaidi wa ujasusi na kunasa sauti na mazungumzo simu za mkononi kwa ushirikiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Gazeti la Lebanon la Al-Binaa limeandika katika ripoti yake siku ya Jumatano, likinukuu habari za kuaminika kwamba: "Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman hivi karibuni alianzisha chombo cha ujasusi na usalama ambacho kiko chini yake moja kwa moja."
Al-Binaa limeongeza kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia ameamuru kuanzishwa mradi uliopewa jina la Al Kahf (pango), ambao kwa hakika ni mfumo wa usalama wa kidijitali, ambao dhamira yake ni kuunganisha laini zote za simu na data kwenye shirika la ujasusi la Saudi Arabia na kudukua na kufuatilia mazungumzo ya watu.
Kwa mujibu wa gazeti la Al-Binaa, mfumo huo wa usalama unazinduliwa kwa ushirikiano wa utawala wa Kizayuni wa Israel ili vyombo vya ujasusi vya Tel Aviv vibadilishane taarifa na Riyadh, na kwamba utawala huo utaweza kupata data na mawasiliano yote haswa data zinazohusiana na Syria na Lebanon.
Gazeti hilo pia limeripoti kuwa, huduma hiyo ya ujasusi ina uwezo wa kufuatilia mawasiliano ya nambari zinazotumiwa katika mitandao ya kigeni kama Telegram, Facebook na SnapChat, na kwamba hatari ya mradi wa Al-Kahf sio ndogo kuliko ile ya programu ya kijasusi ya Kizayuni ya Pegasus.
Uchunguzi wa mashirika zaidi ya 17 ya habari inaonesha kuwa, programu ya kijasusi ya Pegasus, iliyotengenezwa na kampuni ya NSO ya Israel, imekuwa ikitumika kujasisi simu za mamia ya waandishi wa habari, wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii, pamoja na wanasiasa duniani kote.
Israel imeuza programu ya kijasusi ya "Pegasus" kwa nchi kadhaa, zikiwemo Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Miongoni mwa wanasiasa ambao simu zao zilidukuliwa kwa kutumia programu ya kijasusi ya Pegasus ni Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.