HAMAS yaionya Israel iache kucheza na moto
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa onyo kali kwa utawala haramu wa Israel baada ya walowezi wake wa Kizayuni kuwashambulia tena Wapalestina katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Indhari hiyo imetolewa leo Jumapili na Muhammad Hamadeh, msemaji wa HAMAS mjini Quds ambaye amebainisha kuwa, “shambulio hilo ni ukanyagaji wa wazi wa sharia, na (Israel) inacheza na moto.”
Hamadeh amesisitiza kuwa: Tunaonya utawala ghasibu (wa Israel) dhidi ya wimbi la mashambulio haya na matokeo yake mabaya, hujuma ambazo ni sawa na kucheza na mada za miripuko ambazo zitauripoukia usoni (utawala huo).
Msemaji huyo wa HAMAS katika mji mtukufu wa Quds ametoa mwito kwa Wapalestina wote kusimam kidete na kuungana mkabala wa utawala huo haramu na walowezi wake waoga.
Makundi ya wanamapambano wa Palestina hivi karibuni pia yalitoa tamko la pamoja na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Baitul Muqaddas na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Makundi hayo ya muqawama ya Palestina yalitoa onyo kali kwa Wazayuni na kusema kuwa, maafa yoyote yatakayotokea kutokana na jinai hizo, lawama zote zitakuwa ni za utawala wa Kizayuni.