Mwanaharakati wa Saudia: Sina amani, naandamwa na makachero wa Bin Salman
Wakati vyombo vya habari vya Saudia na makampuni ya mahusiano ya umma katika nchi za Magharibi, yaliajiriwa na serikali ya Riyadh yakiendelea kusafisha na kupendezesha sura ya mrithi wa ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman, iliyochafuliwa na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi, mwanaharakati wa Kisaudia Alya Alhwaiti anayeishi London, amelipua bomu baada ya kufichua kwamba alipokea vitisho vya kuuawa.
Alya Alhwaiti amesema katika mahojiano na gazeti la Uingereza Independent kwamba ameweka kengele ya tahadhari nyumbani kwake mjini London baada ya kupokea vitisho vya kuuliwa na kudukuliwa baruapepe zake, kwa sababu ya kukosoa ukandamizaji unaofanywa na Bin Salman dhidi ya wapinzani wake.
Alya, 36, ambaye mwaka 2005 alikua mpanda farasi wa kwanza wa kike wa kimataifa wa nchi yake, ameongeza kuwa Riyadh imemkasirikia kutokana na ukosoaji wake wa hadharani dhidi ya Bin Salman kufuatia mauaji ya Jamal Khashoggi ambaye aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul mwaka 2018, na vilevile kwa sababu ya kampeni yake ya kuliunga mkono kabila la Al-Huwaitat linalofukuzwa katika makazi yake huko kaskazini mwa Saudia.
Mwanaharakati huo amesema, amekuwa akipokea vitisho kupitia mitandao ya kijamii na kwa njia ya simu akiambiwa kuwa asidhani kwamba ana amani mjini London.
Amesema amepokea jumbe mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii akitishiwa kupigwa risasi kichwani. Mwanaharakati huo amesisitiza kuwa, wanaomtumia ujumbe wa vitisho wako katika kituo cha masuala ya usalama wa ndani mjini Riyadh ambacho kinasimamiwa na watu wa karibu kwa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman.
Mwanamfalme wa Saudi Arabia na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Muhamamd Bin Salman amekuwa akitumia mbinu ya mauaji kuwamaliza wapinzani wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo.
Mwezi Agosti mwaka 2020 Mahakama ya Washington DC ilimtaka mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na wenzake 13 kufika mahakamani kujibu tuhuma za kufanya jaribio la kutaka kumuua kigaidi Saad al Jabri, mkuu wa zamani wa Idara ya Intelijensia la Saudi Arabia aliyekimbilia nchini Canada.
Saad al-Jabri, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Canada na anayejulikana kama "Kisanduku Cheusi cha Aal Saud", ana nyaraka muhimu zinazomhusu mfalme Salman bin Abdul-Aziz pamoja na mwanawe, Muhammad bin Salman ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ambapo kama nyaraka hizo zitavuja na kusambazwa zinaweza kuharibu mno sura ya bin Salman ulimwenguni.