Imarati inawajengea vitongoji askari wa Israel huko Socotra, Yemen
(last modified Wed, 09 Mar 2022 10:42:37 GMT )
Mar 09, 2022 10:42 UTC
  • Imarati inawajengea vitongoji askari wa Israel huko Socotra, Yemen

Umoja wa Falme za Kiarabu umeripotiwa kujenga vitongoji katika kisiwa cha kistratijia cha Yemen cha Socotra ambacho kinakaliwa kwa mabavu na Imarati, kwa ajili wanajeshi wa utawala haramu wa Israel; zaidi ya mwaka mmoja baada ya tawala hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kawaida.

Tovuti ya habari ya "Yemen News Portal" imenukuu vyanzo vya habari ambavyo havikutaka kutajwa majina vikisema kuwa, Taasisi ya Khalifa bin Zayed ya UAE imezindua mpango wa kuwajengea nyumba askari wa utawala haramu wa Israel katika kambi ya pamoja na Imarati na Israel kisiwani Socotra.

Duru hizo za habari zimearifu kuwa, ujenzi huo wa nyumba za makazi ya watu unaenda sambamba na jitihada za Imarati za kuzihamishia Yemen familia za askari wa Israel walioko Socotra. Madazeni ya familia za Kizayuni zimewasili Socotra katika wiki za hivi karibuni, wakijifanya kuwa watalii.

Januari mwaka huu, Wayemen walighadhabishwa mno na kitendo cha kuenea picha zinazowaonyesha "watalii" kutoka utawala haramu wa Israeli wakitembelea kisiwa hicho cha kistratijia cha Yemen. Wananchi wa Yemen wanasisitiza kuwa, UAE inakiuka sheria za kimataifa kwa kuzingatia kuwa Socotra ni kisiwa cha Yemen kinachokaliwa kwa mabavu na Imarati.

Kisiwa cha Socotra cha Yemen inachokaliwa kwa mabavu na UAE

Serikali ya Wokovu wa Kitaifa yenye makao yake Sana'a imelaani vikali hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwaingiza Waisraeli katika Kisiwa cha Socotra. Taarifa zinadokeza kuwa UAE ikishirikiana na utawala haramu wa Israel inalenga kujenga kituo cha kijasusi katika kisiwa hicho cha Yemen.

Socotra ni kisiwa chenye wakazi 60,000 katika eneo muhimu la baharini la Lango Bahari la Bab el Mandeb ambalo linaunganisha Bahari ya Sham na Ghuba ya Aden pamoja na Bahari Arabu.