Saudi Arabia na kuongeza gharama za kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81226-saudi_arabia_na_kuongeza_gharama_za_kijeshi
Walid Abu Khalid, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwanda vya Silaha vya Saudi Arabia ametangaza kuwa, taifa hilo la Kiarabu lina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa zaidi ulimwenguni cha utengenezaji na uzalishaji silaha na zana za kijeshi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2022 07:10 UTC
  • Saudi Arabia na kuongeza gharama za kijeshi

Walid Abu Khalid, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwanda vya Silaha vya Saudi Arabia ametangaza kuwa, taifa hilo la Kiarabu lina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa zaidi ulimwenguni cha utengenezaji na uzalishaji silaha na zana za kijeshi.

Saudia ni nchi ya tatu ulimwengu kwa kuwa na bajeti kubwa zaidi ya kijeshi. Ni Marekani na China tu ndizo zinazoipiku Saudia katika kuwa na bajeti kubwa ya kijeshi. Kuhusiana na gharama za kijeshi za Saudia kuna nukta kadhaa ambazo kuna udharura wa kuzitaja naa kuzibainisha.

Mosi; kukabidhiwa Wizara ya Ulinzi ya Saudia Muhammad bin Salman ambaye pia ni mrithi wa kiti cha ufalme kulikwenda sambamba na kuongezeka bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.

Pili; Baraza la Mawaziri la Saudi Arabia mwaka huu wa 2022 limetenga bajeti ya kiasi cha riali bilioni 171  za Saudia (sawa na takribani dola bilioni 46) kwa ajili ya sekta ya kijeshi. Gazeti la Financial Times hivi karibuni liliashiria gharama kubwa ya kijeshi ya Saudia na kuandika kwamba, nchi hiyo ni moja ya mataifa yenye bajeti kubwa zaidi ya kijeshi ulimwenguni.

Saudia imekuwa ikinunua sehemu kubwa ya silaha zake kutoka Marekani

 

Tatu; sehemu ya bajeti ya jeshi ya Saudia ambayo inahusiana na manunuzi ya silaha na vilevile gharama za vita haijumuishwi katika bajeti ya kijeshi.

Nne; Saudia ndio nchi inayoshika nafasi ya kwanza duniani kwa kununua silaha ambapo sehemu kubwa ya silaha hizo zinaingizwa na kuagiziwa kutoka Marekani. Katika kipindi kati ya mwaka 2016 na 2020 Saudia ilinunua 24% ya silaha zote zilizouzwa na Marekani.

Gazeti la al-Khalij Online liliandika katika ripoti yake ya mwezi uliopita wa Februari kwamba, Saudia ni mmoja wa wanunuzi wakubwa zaidi wa silaha duniani, ambapo katika kipindi cha miaka 5 iliyopita imeshikilia rekodi ya 11% ya uingizaji silaha duniani huku 79% ya silaha hizo ikizinunua kutoka Marekani.

Tano; licha ya Saudia kutumia gharama kubwa kiasi hiki kwa ajili ya masuala ya kijeshi, lakini inakabiliwa na tatizo la kuweza kudhurika kijeshi na kutokuwa na usalama. Kuna sababu mbalimbali kuhusiana na hili. Moja ya sababu muhimu zaidi ni kuwa, sehemu ya sekta ya kijeshi ya Saudia ina mfungamano na utegemnezi mkubwa kutoka nje.

Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme Saudia

 

Hii ni kutokana na kuwa, kimsingi utawala wa Aal Saud unaamini suala la usalama wa kuagizia kutoka nje. Katika hali ambayo, kunatumika bajeti kubwa kwa ajili ya masuala ya kijeshi, lakini sekta ya kijeshi ya nchi hiyo ni dhaifu mno.

Kuhusiana na hilo, weledi wa mambo wanaashiria mashambulio ya ndege zisizo na rubani (droni) na makombora ya Wamayen dhidi ya  taasisi za shirika kubwa zaidi la mafuta la Saudi Arabia la Aramco na miundomsingi ya nchi hiyo.

Ukweli wa mambo ni kuwa, licha ya Saudia kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kununua aina kwa aina ya silaha na zana lukuki za kijeshi, lakini nchi hiyo imeshindwa kupata mafanikio yoyote katika hujuma yake dhidi ya nchi masikini zaidi ya Kiarabu ya Yemen, kwani licha ya kupita miaka saba tangu ianzishe hujuma yake ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo tena ikishirikiana na washirika wake, lakini hivi sasa imekwama katika kinamasi cha Yemen na viongozi wa nchi hiyo wamediriki kuwa, Yemen ni tonge ambalo halimezeki kirahisi.

Wakati huo huo, Ahmad al-Uhali, Mkuu wa Shirika la Viwanda vya Silaha vya Saudi Arabia ametangaza kuwa, nchi hiyo itaendelea kuifanya sekta ya viwanda vya kijeshi na kiusalama kuwa vya kitaifa na mpaka kufikia mwaka 2030 gharama za kijeshi kwa ajili ya zana na huduma za kijeshi itaongezeka kwa 50%.

Saudia imekuwa ikitumia silaha inazonunua kwa ajili ya kufanya mauaji nchini Yemen

 

Naye Walid Abu Khalid, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwanda vya Silaha vya Saudi Arabia sambamba na kuashiria kwamba, mpaka kufikia mwaka 2030 zaidi ya 50 ya zana za kijeshi za nchi hiyo zitakuwa zikitengenezwa ndani ya Saudia amesema kuwa, Shirika la Viwanda vya Kijeshi la Saudi Arabia linashirikiana na mashirika ya ndani kwa ajili ya kubuni ndege 100 zisizo na rubani (drone) ambazo 100% ya mchakato wa uundaji wake utategemea teklonojia na wataalamu wa ndani ya nchi.

Drone hizo zitakuwa zikizalishwa na kutumiwa na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo. Hata kama kuifanya sekta ya zana za kijeshi itegemee wataalamu wa ndani ni hatua ya kimkakati na inalenga kuinua uwezo wa kiulinzi wa Saudia, lakini katika upande mmoja, kunaonyesha kutokuwa sahihi mkakati wa nchi hiyo wa kuingiza bila mpango silaha za madola ya Magharibi na kwa upande mwingine hilo linapelekea kuongezeka gharama za kijeshi za taifa hilo la Ghuba ya Uajemi. Hii ni katika hali ambayo, matatizo ya kiuchumi ya Saudia yameshadidi ikiwa ni natija na matokeo ya sera zake ghalati za kupenda vita hususan katika vita vya miaka 7 ilivyovianzisha dhidi ya taifa masikini la Kiarabu la Yemen.