Umuhimu wa safari ya Bashar al Assad huko Imarati
Rais wa Syria Bashar al-Assad Ijumaa iliyopita alifanya ziara yake ya kwanza katika nchi ya Kiarabu baada ya miaka 11. Assad alitembelea nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika ziara ambayo imewashangaza wengi na kuikasirisha mno serikali ya Marekani
Safari ya Assad nchini Imarati (UAE) ni muhimu katika pande kadhaa:
Kwanza ni kwamba Safari hiyo imekamilisha kushindwa kwa juhudi za kijeshi na kisiasa za kutaka kuangusha utawala wa Syria. Mwezi Februari 2012 UAE na nchi nyingine tano za wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi ziliwarejesha nyumbani mabalozi wao waliokuwa nchini Syria. UAE pia imetumia pesa nyingi katika muongo mmoja uliopita kwa shabaha ya kupindua serikali ya Syria inayoongozwa na Rais Bashar al-Assad. Hata hivyo, Imarati sasa imekuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu kumwalika Bashar al-Assad baada ya miaka 11, na Rais huyo wa Syria alikaribishwa na Mwanamfalme wa UAE, Mohammed bin Zayed al Nahyan. Bin Zayed huyo aliyekwenda kumlaki Rais Assad, alikuwa mwanzilishi wa harakati na njama mbalimbali dhidi ya Syria katika ulimwengu wa Kiarabu kwa muda wa miaka 11 iliyopita. Katika kipindi hicho chote Bashar al-Assad amesafiri mara chache nje ya nchi na ametembelea Russia na Iran pekee, washirika wawili wa Syria katika mapambano dhidi ya magaidi na waungaji mkono wa ugaidi.

Pili ni kwamba, zara ya Bashar al-Assad huko Imarati ni kukiri na kukubali uhalali wake katika muundo wa mamlaka ya Syria. Jambo muhimu katika uwanja huu ni kwamba, Bashar al-Assad amefanya safari huko Imarati mwezi huu wa Machi, katika kumbukumbu ya miaka 11 ya vita vya ndani nchini Syria vilivyoanza Machi mwaka 2011. Ujumbe wa safari hii ni kwamba, Bashar al-Assad ametangaza ushindi dhidi ya wapinzani wake na kufikisha ujumbe kwamba, kama alivyokubaliwa na watu wa Syria katika uchaguzi wa rais wa Mei 2021, sasa uhalali wake kama kiongozi wa Syria, umetambuliwa rasmi na nchi za kigeni. Suala hili ndio sababu ya hamaki na hasira kubwa ya Marekan dhidi ya Imarati kutokana na kumwalika Assad huko Abu Dhabi. Televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar imemnukuu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani akisema: "Tunasikitishwa na juhudi za kuhalalisha utawala wa Bashar al-Assad."
Tatu ni kwamba, bado haijabainika iwapo Syria itarejea katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) au la. Syria ilifukuzwa kwenye jumuiya mwishoni mwa 2011. Baadhi ya nchi za Kiarabu kama Imarati, Algeria na Kuwait zimetoa wito wa kurejeshwa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, japokuwa nchi za Saudi Arabia na Qatar zinapinga suala hilo. Safari ya Bashar al Assad huko Imarati, kama sio utangulizi wa kuirejesha Syria kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kumaliza mpasuko ndani ya jumuiya hiyo kuhusu Syria, basi ina maana kwamba, nchi wanachama wa Arab League zimeamua kuhuisha uhusiano wao na na Damascus, kila moja kivyakevyake.

Nne ni kwamba, mwaliko wa Mohammad bin Zayed kwa Bashar al-Assad kutembelea Imarati una maana kwamba, Abu Dhabi inataka kupanua uhusiano na Damascus. Uhusiano wa UAE na Syria ulikatwa kwa upande mmoja na Imarati tangu 2011, lakini mwishoni mwa 2018, Abu Dhabi ilifungua tena ubalozi wake mjini Damascus. Novemba mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan alikutana na Rais wa Syria mjini Damascus kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita nchini Syria. Inaonekana kwamba, kwa upande mmoja, Imarati inajaribu kuwa na nafasi ya kiuchumi na kuwekeza nchini Syria baada ya zaidi ya muongo mmoja wa harakati za kigaidi zinazofadhiliwa na madola ya Magharibi na waitifaki wao wa kikanda; na kwa upande mwingine, inajaribu kujenga upya sura yake iliyoharibiwa na kuchafuka kama nchi inayounga mkono ugaidi.