Mwisho wa Abdrabbuh Mansur Hadi; hatima ya kila msaliti, mamluki
Ushahidi unaonesha kuwa Saudi Arabia imeamua kumpiga teke Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu mwenyewe na kukimbilia Saudia kushirikiana na wavamizi wa nchi yake. Kuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa Riyadh imemtupa nje ya ulingo wa siasa Mansur Hadi.
Kuanzia mwaka 1994 hadi 2012, yaani kwa muda wa miaka 18, Abdrabbuh Mansur Hadi alikuwa Makamu wa Rais Ali Abdallah Saleh wa Yemen. Mwaka 2012 Mansur Hadi alichukua madaraka ya Yemen baada ya kupinduliwa Ali Abdallah Saleh. Aliingia madarakani katika uchaguzi wa kimaonesha ambao haukuwa na upinzani wowote.
Ilivyokuwa imepangwa kikatiba ni kwamba Mansur Hadi awe rais wa mpito nchini Yemen kwa muda wa miaka miwili tu. Lakini mwaka 2014 yaani ulipoisha muda wake, aliamua kung'ang'ania madaraka na alijiongezea muda wa mwaka mzima wa kubakia madarakani kinyume cha sheria. Hata baada ya kumalizika mwaka huo mmoja aliokuwa amejiongezea kinyume cha Katiba, Mansur Hadi bado hakutaka kukabidhi madaraka. Mwaka 2015 baada ya kumalizika muda aliojiongezea madaraka, alilazimika mwenye kutangaza kujiuzulu lakini nia yake haikuwa kukabidhi madaraka kwa serikali ambayo ingelichaguliwa kidemokrasia hivyo aliamua kukimbilia Saudia.
Baada ya hapo alishirikiana na wavamizi wa Yemen ambao walidai kuwa lengo lao ni kumrejesha madarakani Mansur Hadi. Kimsingi ni usaliti na umamluki wa Mansur Hadi ndio ulioitumbukiza Yemen kwenye vita angamizi vya maadui kwa zaidi ya miaka saba sasa.
Ijapokuwa Saudia na wavamizi wenzake wangelitafuta kisingizio chochote tu cha kuivamia Yemen bila ya kusubiri idhini kutoka kwa Mansur Hadi, lakini kuweko kwake Mansur Hadi huko Riyadh, Saudi Arabia ni uungaji mkono tosha wa kuvamiwa na kuuliwa kiholela wananchi wa Yemen. Mansur Hadi alikuwa na ndoto za kurejea madarakani nchini Yemen na kwake si muhimu ni idadi ngapi ya watu wangeliuawa na uharibifu mkubwa kiasi gani ungelifanywa na wavamizi wasioipendelea kheri yoyote Yemen zaidi ya kujali maslahi yao binafsi tu.
Hivi sasa muda wa matumizi ya Mansur Hadi unaonekana umeisha. Ushahidi ni kuwa, Jumatano ya wiki iliyopita, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi lilianzisha mazungumzo mjini Riyadh kwa ajili ya Yemen. Hata hivyo katika kikao cha ufunguzi wa mazungumzo hayo, si Abdrabbuh Mansur Hadi alikuwepo wala makamu wake, Muin Abdul Malik ambaye pia ni waziri mkuu wake. Vyombo vya habari vya Yemen vilitangaza kuwa, kukosekana Mansur Hadi katika kikao hicho cha ufunguzi ni ushahidi kuwa ukoo wa Aal Saudi umeamua kumtupa nje ya ulingo wa siasa Mansur Hadi ambaye kwa miaka mingi sasa anaishi kwa fadhila za ukoo huo huko Saudia. Taarifa nyingine zinasema kuwa, Mansur Hadi haruhusiwi hata kuwa na mazungumzo yoyote ya kisiasa, wala kuhojiwa na vyombo vya habari na wala kuonana na wakuu wa nchi za dunia. Mujtahid, mfichuaji maarufu wa siri zinazopitikiana ndani ya ukoo wa kifalme wa Aal Saud ameandika katika Twitter kwamba, baadhi ya duru za kuaminika zimesema kuwa, balozi wa Saudia nchini Yemen amempiga marufuku Mansur Hadi kuzungumza na vyombo vya habari kwa namna yoyote ile. Kwa matamshi hayo tunaweza kusema kuwa, mchezo umekwisha na Mansur Hadi ameshatupwa tayari katika kapu la historia.
Jambo jingine muhimu ni kwamba Saudia haiamiliani kwa heshima na Mansur Hadi tofauti na inavyomfanyia Meja Jenerali Aidarus al Zoubaidi, mkuu wa baraza la mpito la kusini mwa Yemen. Jenerali al Zoubaidi ni kibaraka wa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kwa vile inaonekana wazi kwamba Imarati ilikuwa na hitilafu tangu mwanzo na Mansur Hadi, imefanikiwa kuitwisha Saudia msimamo wake wa kutaka Mansur Hadi atupwe nje ya ulingo wa siasa.
Ijapokuwa bado haijatangazwa rasmi kuwa Mansur Hadi ameshapigwa teke, lakini vitendo vya ukoo wa Aal Saud katika miaka ya hivi karibuni hasa mwaka wa saba wa uvamizi wa Yemen vinaonesha madharau makubwa kwa Mansur Hadi. Lakini hilo si jambo la kushangaza kwani huo ndio mwisho wa msaliti yeyote yule.