HAMAS yatoa mwito kwa Wapalestina kusimama imara kukabiliana na Wazayuni
(last modified Thu, 14 Apr 2022 10:24:28 GMT )
Apr 14, 2022 10:24 UTC
  • HAMAS yatoa mwito kwa Wapalestina kusimama imara kukabiliana na Wazayuni

Naibu wa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema baada ya Wazayuni kuwaua shahidi vijana wanne wa Kipalestina kwamba wananchi wote wa Palestina wanapaswa kusimama imara kupambana kiume na Wazayuni.

Televisheni ya al Mayadeen imetangaza hayo leo na kumnukuu Saleh al Arouri akiwataka Wapalestina kuwa imara zaidi katika kukabiliana na mashambulizi ya wanajeshi wa Israel ambao hivi sasa wanaishambulia mfululizo miji na vitongoji mbalimbali vya Wapalestina. 

Katika siku za karibuni wanajeshi makatili wa Israel wamekuwa wakivamia mtawalia maeneo ya Wapalestina hususan mji wa Jenin wa kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na hadi hivi sasa wameshawaua shahidi vijana wanne wa Kipalestina na kuwajeruhi makumi ya wengine.

Saleh al Arouri

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa harakati ya Palestinian Initiative, Mustafa Barghouthi amesema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu unamwaga daumu za Wapalestina katika njama za kuficha kushindwa kwake kisiasa na kiusalama.

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni siku kadhaa zilizopita waliishambulia kambi ya wakimbizi ya Jenin, Kaskazini ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kuwauwa shahidi Wapalestina wanne na kuwajeruhi makumi ya wengine. 

Jana Jumatano, makundi mbalimbali ya mapambano ya Palestina yaliitisha kikao cha dharura mjini Ghaza kutokana na kuongezeka mno uhalifu na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, kikao hicho cha dharura cha makundi ya muqawama ya Palestina kilifanyika jana usiku kujadili jinai hizo za Wazayuni katika mji wa Jenin na dhidi ya Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Tags