Jeshi la Israel lamuua shahidi mwanamke wa Palestina
Askari wa jeshi katili la utawala haramu wa Israel wamemuua shahidi mwanamke wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hii leo.
Habari zinasema kuwa, jeshi hilo limemuua mwamke huyo wa Kipalestina kwa kummiminia risasi katika eneo la Anabta, karibu na mji wa Tulkarm, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, kwa tuhuma za kujaribu kumdunga kisu askari wa utawala huo ghasibu. Errab Foqoha, Msemaji wa Shirika la Hilali Nyekundu amesema jeshi la Israel limezuia ambulensi kufika katika eneo la tukio ili kumbemba mwanamke huyo aliyepigwa risasi kabla hajakata roho.
Mbali na wanawake, jeshi katili la utawala wa Kizayuni wa Israel limekuwa likiwalenga watoto wadogo katika hujuma zake hizo za kutisha. Jana Jumatano, Wizara ya Habari ya Palestina ilitangaza katika ripoti yake kuwa tangu kuanza Intifadha ya Masjidul Aqsa mwaka 2000 hadi sasa, watoto wa Kipalestina 2079 wameshauliwa shahidi na wanajeshi wa Kizayuni huku wengine 1300 wakijeruhiwa.
Hii ni katika hali ambayo Intifadha Mpya ya Palestina yaani Intifadha ya Quds ilianza mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana kufuatia siasa za kichokozi na ukandamizaji zinazofanywa na utawala wa Kizayuni sambamba na njama zake za kutaka kubadili utambulisho wa Baitul Muqaddas na mpango wake wa kutaka kuugawa msikiti wa al Aqsa kwa mujibu wa wakati na kieneo. Wapalestina 250 wameuliwa shahidi hadi sasa katika Intifadha hiyo.