Al-Houthi: Marekani inasaidiana na magaidi kujenga vituo vya kijeshi Yemen
(last modified Sat, 21 May 2022 03:54:39 GMT )
May 21, 2022 03:54 UTC
  • Al-Houthi: Marekani inasaidiana na magaidi kujenga vituo vya kijeshi Yemen

Kiongozi wa harakati ya wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema Marekani, ikishirikiana na magaidi wakufurishaji ambao ni waitifaki wake, inajenga vituo kadhaa vya kijeshi katika mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo ya Hadhramaut na al-Mahrah na hali kadhalika mji wa Aden na pwani ya Bahari ya Sham.

Akihutubia ujumbe wa viongozi wa kikabila kutoka mkoa wa magharibu mwa Yemen wa Ibb Alhamisi jioni, Sayyid Abdul-Malik Badruldeen al-Houthi ameashiria ujenzi wa vituo hivyo vya kijeshi vya Marekani nchini humo na kusema Wayemen hawatakubali kupokea amri kutoka Washington. Aidha ametahadharisha kuwa maadui wanafanya juu chini kuibua mifarakano na migawanyiko baina ya watu wa Yemen.

Al Houthi amesema maadui sasa wanatumia fursa iliyojitokeza ya usitishwaji vita unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa kujitayarisha kwa awamu nyingine ya vita kwa sababu walifeli katika miaka iliyopita.

Katika matamshi yake mengine, kiongozi wa Ansarullah ameashiria mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu na kusema mapatano kama hayo yatatoa mwanya kwa utawala wa Tel Aviv kujipenyeza zaidi Asia Magharibi.

Amesema nchi za Kiarabu ambazo zimepatana na Israel ndizo zinaonyesha uadui na kutekeleza hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen. Amesema maadui wanalenga kuvuruga umoja wa Yemen lakini Wayemen watendelea katika mkono wao wa uhuru na kujitegemea na hawatawaruhusu wageni waingilie mambo yao ya dani.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE na kwa himaya ya Marekani na utawala haramu wa Israel na madola mengine ya Magharibi ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Vita vilivyoanzishwa  na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen na kuendelea hadi sasa vimeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha mamilioni wakiwa hawana pa kuishi. Aidha vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya ukosefu wa chakula, matibabu na elimu kwa watu wa Yemen.

Katika kulipiza kisasi jinai hizo, Jeshi la Yemen hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo ya kistratijia ya Saudi Arabia na UAE.