Muqawama wa Palestina: Maandamano ya bendera ya Wazayuni yatawasha moto
Makundi mbalimbali ya mapambano ya Kiislamu ya Palesitna yametoa mwito kwa Wapalestina kujitokeza kwa wingi kuulinda Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu, kama ambavyo pia yameonya kuhusu hatari ya maandamano ya bendera ya utawala wa Kizayuni kwa usalama wa eneo hili.
Kwa mujibu wa redio ya Sauti ya Quds, makundi ya muqawama ya Palestina usiku wa kuamkia leo Ijumaa yameitisha kikao cha dharura na kutoa tamko la pamoja na kusema kuwa, makundi hayo ya mapambano ya Wapalestina yanafuatilia kwa karibu vitendo vya ukatili na kivamizi vya Israel na kwamba utawala huo pandikizi ndio utakaobeba dhima ya lolote litakalotokea kwenye eneo hili.
Maandamano ya bendera ya utawala wa Kizayuni hufanyika tarehe 10 Mei kila mwaka kwa mnasaba wa kuanza kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni eneo la kale la mji mtukufu wa Baytul Muqaddas.
Wazayuni wanadai kuwa, mji wa Quds eti ndio mji mkuu wa utawala huo pandikizi. Lakini wananchi wa Palestina wanasema kuwa, Quds ndio mji mkuu wa nchi ya Palestina na kwamba upotoshaji wowote ule hauwezi kufifiliza wala kusahaulisha uhakika huo.
Katika taarifa yao, makundi ya muqawama ya Palestina yamewataka Wapalestina wanaoshi katika mji wa Quds, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni wajitokeze kwa wingi kwenye Msikiti wa al Aqsa leo Ijumaa na wakilinde kwa nguvu zao zote Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu.
Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni, gazeti la Maariv la utawala wa Kizayuni lilikiri kuwa Israel haiwezi kukabiliana na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kwenye Ukanda wa Ghaza.