Wayemeni watumia makombora kufikisha chakula maeneo yaliyowekewa mzingiro
Wayemen wamebuni njia mpya ya kufikisha misaada ya chakula kwa raia waliowekewa mzingiro katika wilaya ya Ad Durayhimi mkoani Al-Hudaydah.
Wilaya ya Ad Durayhimi katika mkoa wa Al-Hudaydah ulioko pwani ya magharibi ya Yemen ni katika maeneo yaliyojumuishwa kwenye makubaliano ya usitishaji vita yaliyosainiwa Desemba 2018 mjini Geneva kati ya wawakilishi wa serikali ya Sana'a na wa serikali iliyojiuzulu ya Abdrabbuh Mansur Hadi (mwitifaki wa Saudi Arabia), lakini hadi sasa vikosi vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umeyakiuka mara mia kadhaa makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne na duru za kijeshi za serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen, jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi zimeanzisha ubunifu mpya wa kufikisha misaada ya chakula kwa raia waliowekewa mzingiro katika wilaya ya Ad Durayhimi wa kufyatua makombora kuelekea mji huo yaliyofungwa vifurushi vya nyama na bidhaa zingine za lazima za chakula.
Duru hizo zimebainisha kuwa, kila siku yanafyatuliwa makombora manane hadi kumi yaliyosheheni vifurushi vya chakula na hadi sasa makombora elfu mbili na mia tano yaliyobeba bidhaa za chakula yameshafyatuliwa kuelekea wilaya hiyo iliyowekewa mzingiro.
Mnamo mwezi Machi 2015, Saudi Arabia, ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande nchi hiyo. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake nchini Yemen hadi sasa umesha sababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Uvamizi wa kijeshi wa Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.../