Yaliyojiri katika kikao cha kwanza cha Bunge la Lebanon
(last modified Fri, 03 Jun 2022 02:41:41 GMT )
Jun 03, 2022 02:41 UTC
  • Yaliyojiri katika kikao cha kwanza cha Bunge la Lebanon

Kikao cha kwanza cha bunge la Lebanon kimefanyika kwa kuchaguliwa Spika na Naibu Spika wa bunge hilo.

Uchaguzi wa bunge la Lebanon ulifanyika tarehe 15 ya mwezi uliopita wa Mei. Kikao cha kwanza cha bunge hilo kilifanyika siku ya Jumatano, yaani takriban siku 17 tangu ulipofanyika uchaguzi wake. Hii inaonyesha kuwa mirengo ya kisiasa ya Lebanon ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha bunge jipya linaanza kazi zake mara moja; na hata tofauti na mivutano iliyopo baina ya makundi ya kisiasa ya nchi hiyo haijawa sababu ya kuchelewesha kuanza shughuli za bunge hilo. Kufanyika kikao cha kwanza cha bunge katika anga tulivu na bila mivutano yoyote ni mafanikio mengine kwa Lebanon baada ya kufanyika uchaguzi. Uchaguzi wenyewe wa bunge wa tarehe 15 Mei, nao pia ulifanyika katika mazingira tulivu na ya kidemokrasia ndani ya nchi hiyo na bila kuzuka mikwaruzano yoyote.

Nabih Berri

Katika kikao cha kwanza cha siku ya Jumatano, Nabih Berri, kiongozi wa harakati ya Amal mwenye umri wa miaka 84 alichaguliwa kwa mara ya saba mfululizo kuwa spika wa bunge la Lebanon. Tangu mwaka 1992 hadi sasa Berri amekuwa akishikilia cheo hicho cha uspika. Mara hii amechaguliwa tena baada ya kujipatia kura 65 kati ya kura zote 128 za wabunge.  Mbali na Berri, Elias Bou Saab, kutoka Harakati Huru ya Kizalendo, naye pia amechaguliwa kuwa naibu spika. Bou Saab alimshinda Ghassan Skaf, aliyegombea unaibu spika kwa tiketi ya chama cha Vikosi vya Lebanon kinachoongozwa na Samir Geagea.

Yaliyojiri siku ya Jumatano ndani ya bunge la Lebanon yamebeba nukta muhimu kadhaa.

Ya kwanza ni kwamba, kinyume na propaganda zilizofanywa dhidi ya bunge jipya la Lebanon baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi, mivutano na mitifuano haitatawala bunge jipya, bali badala yake, mshikamano na mashauriano yanayohitajika kwa ajili ya kufanikisha masuala muhimu ya nchi yatatawala ndani ya bunge hilo.

Uchaguzi wa bunge la Lebanon

Nukta ya pili ni kwamba, waitifaki wa Hizbullah ndio waliofanikiwa kushika nyadhifa za uspika na unaibu spika. Harakati ya Kishia ya Amal na Harakati Huru ya Kizalendo zote mbili ni waitifaki wa Hizbullah ambao wamo ndani ya muundo wa madaraka wa Lebanon. Na ndio maana baada ya kikao cha Jumatano cha bunge, vyombo vya habari vya Kiebrania vyenye mfungamano na utawala wa Kizayuni vilikiri kuwa, matokeo ya kikao cha kwanza cha bunge la Lebanon ni ya ushindi na mafanikio kwa waitifaki wa Harakati ya Hizbullah.

Nukta ya tatu ni kuwa, yaliyojiri Jumatano ndani ya bunge la Lebanon yameonyesha kwamba, vita vya kisaikolojia vilivyoanzishwa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi kwamba Hizbullah imeshindwa, zimefeli na kugonga mwamba ndani ya muda mfupi kabisa. Kusema kweli, kura alizopigiwa Nabih Berri na wabunge 65 zinamaanisha kuwa, Hizbullah na waitifaki wake wangali ndio wenye viti vingi zaidi bungeni. Shirika la habari la Ujerumani limeeleza katika uchambuzi wake kuwa, matukio ya kikao cha kwanza cha bunge la Lebanon ni kielelezo cha ushindi kwa Hizbullah.

Na nukta ya nne na ya mwisho ni kwamba, licha ya propaganda chungu nzima zilizofanywa kuhusu nafasi ya chama cha Vikosi vya Lebanon kinachoongozwa na Samir Geagea katika bunge jipya la Lebanon, katika hatua yake ya kwanza tu chama hicho kimepigwa mweleka. Kushindwa chama cha Vikosi vya Lebanon ni sawa na kushindwa pia Saudi Arabia na Marekani; kwa sababu wao walikuwa ndio waungaji mkono wakuu wa mrengo huo na walijaribu kuonyesha kwamba chama cha Vikosi vya Lebanon na kiongozi wake Geagea ni washindani wakuu wa Hizbullah na waitifaki wake.../