Haniya: Mapambano yataendelea mpaka Palestina iliyoanzia kwenye Mto hadi Baharini itakapokombolewa
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, mapambano na muqawama ungali unaongeza nguvu zake hadi ufike wakati wa kukombolewa Palestina iliyoanzia Mto Jordan hadi Bahari ya Mediterania.
Wananchi na makundi ya Wapalestina yanasisitiza kutumia muqawama na mapambano kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi na ukaliaji kwa mabavu wa ardhi zao unaofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na wanaamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kukabiliana na ughasibu wa utawala huo.
Ismail Haniya, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, aliyekuwa akihutubia kongamano la mirengo ya kitaifa na Kiislamu linalofanyika katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut ameeleza katika hotuba yake kwamba, Saiful-Quds (Upanga wa Quds) ni nukta yenye umuhimu wa kipekee katika mchakato na vuguvugu la mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Haniya amesisitiza kwa kusema: "sisi tunawajua vizuri maadui, tumepigana vita nao magerezani na kwenye mitaa ya Palestina na hii leo muqawama wa Palestina umefikia hatua ya kuufanya utawala wa Kizayuni usithubutu kuanzisha hujuma".
Kiongozi huyo wa Hamas ametahadharisha pia kuhusu hatari ya utawala wa Kizayuni kujumuishwa kwenye miungano ya kijeshi ya ukanda huu na akaongezea kwa kusema: "inapasa medani zote za mapambano na kambi zote za muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni ziungane na kuwa kitu kimoja".
Ismail Haniya amezungumzia pia ukiukaji wa mipaka ya bahari ya Lebanon unaofanywa na utawala wa Kizayuni na akasisitiza kwa kusema: "sisi tunaiunga mkono Lebanon katika kunufaika na haki yake katika Bahari ya Mediterania".
Kuhusu matukio yanayoendelea kujiri katika eneo, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema: "kinachoendelea kujiri katika eneo ni hatari kubwa zaidi kuliko kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni".../