Saudia inakaribia kuwanyonga vijana watano raia wa nchi hiyo
Utawala wa Aal Saud unaendelea kutekeleza vitendo vyake viovu na vilivyo kinyume cha sheria kwa kuwafunga jela raia kinyume cha sheria kutokana na umri wao mdogo, kwa tuhuma zisizo na msingi.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekosoa mara nyingi ukiukaji mkubwa unaoshuhudiwa katika idara ya mahakama na vyombo vya sheria vya Saudi Arabia. Wale wanaotuhumiwa kwa uhalifu na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na watoto mara nyingi haki zao hukiukwa ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.
Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa, vijana 5 kati ya 21 wa Kisaudi ambao wamefungwa jela wamehukumiwa kunyongwa na serikali ya utawala wa Aal Saud. Hii ni katika hali ambayo, maafisa husika wa nchi hiyo mwaka 2020 walitangaza katika sehemu moja ya dikrii za kifalme kwamba, watafuta hukumu ya kifo kwa wale waliopatwa na hatia ya kutenda uhalifu wakiwa na umri mdogo.
Aidha Juni 15 mwaka jana, mtoto kwa jina la Mustafa al-Darwish alinyongwa baada ya Tume ya Haki za Binadamu ya Saudia kutangaza tarehe 14 Mei kupitia dikrii hiyo ya kifalme kufuta hukumu zote za kunyongwa watoto walio chini ya umri wa kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria. Hivi karibuni pia Mahakama ya Rufaa ya Saudi Arabia ilipasisha hukumu ya kunyongwa raia wa nchi hiyo kwa jina la Haidar Nasser al Thaifah mwenyeji wa mji wa Qatif nchini humo.
Jumuiya na makundi mengi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu khususan huko Marekani na Ulaya yameeleza wasiwasi wao kuwa uwepo wa ombwe katika sheria za Saudi Arabia kunatoa mwanya kwa majaji wa nchi hiyo kuendelea kutoa hukumu za kifo kwa mabarobaro.