Hamas yapinga misimamo ya Saudia ya kujikurubisha zaidi kwa wazayuni maghasibu
(last modified Sat, 16 Jul 2022 02:55:19 GMT )
Jul 16, 2022 02:55 UTC
  • Hamas yapinga misimamo ya Saudia ya kujikurubisha zaidi kwa wazayuni maghasibu

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepinga vikali hatua ya Saudi Arabia ya kufungua anga ya nchi hiyo kwa ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hamas imepinga uamuzi wa Saudi Arabia wa kufungua anga yake kwa ndege za utawala wa haramu wa Israel na kutangaza kuwa, hatua hiyo ya Saudia itaendeleza hatua za kiuadui za utawala wa Kizayuni dhidi ya Palestina na Umma wa Kiislamu.

Harakati ya Hamas imesisitiza kuwa, kufunguliwa anga ya Saudia kwa ndege za utawala wa Kizayuni ni sawa na kuupongeza utawala huo kwa kuivamizi Quds tukufu.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina pia kwa mara nyingine imetangaza upinzani wake dhidi ya mchakato wa kuhalalisha na juhudi za kuanzisha uhusiano baina ya nchi za Kiarabu na adui wa Umma wa Kiislamu ambaye anafanya jinai za kutisha na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina.

Baada ya Saudi Arabia kuruhusu utawala haramu wa Israel kutumia anga yake, ndege iliyokuwa imembeba Rais Joe Biden wa Marekani ilikuwa safari ya kwanza rasmi moja kwa moja baina ya Israel na Saudia. 

Biden aliwasili Jiddah jana Ijumaa akitokea Israel na kufanya mazungumzo na Mfalme wa Saudia, Salman bin Abul Aziz ambayo pia yamehudhuriwa na mrithi wa utawala huo, Muhammad bin Salman ambaye vyombo vya ujasusi vya Marekani, ikiwemo CIA vilimtangaza kuwa ndiye aliyepanga na kuamuru mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala huo, Jamal Khashoggi akiwa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul tarehe Pili Oktoba mwaka 2018.

Biden na Bin Salman

Wakati huo Biden aliwaambia Wamarekani kuwa mauaji ya mwandishi huyo wa habari katika ubalozi wa Saudia nchini Uturuki yanaleta udharura wa kutengwa utawala wa Riyadh katika medani ya kimataifa. Biden aliahidi kuwa atahakikisha kuwa suala hilo linafanyika. Vilevile aliilaumu Saudi Arabia kwa kukosa utu na kuwa kinara wa kuvunja haki za binadamu.

Tags