Jul 22, 2022 02:32 UTC
  • Mafanikio ya mkutano wa Tehran katika matamshi ya Erdoğan

Kama ilivyotazamiwa, Mkutano wa 7 wa "Dhamana ya Mchakato wa Astana" uliofanyika majuzi mjini Tehran umekuwa na mafanikio makubwa kuhusu masuala yanayohusiana na serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria na watu wa nchi hiyo.

Kuhusiana na suala hili, hasa maagizo ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei, kwa viongozi wa nchi za mchakato wa Astana, yamekuwa yenye ufanisi na taathira kubwa, na kwa namna fulani, ni msimamo wa mwisho kwa serikali ya Syria na nchi zinazohusika katika masuala ya nchi hii, na hata harakati za kigaidi zenye mfungamano na Magharibi.

Katika mkondo huo, siku ya Jumatano (Julai 20), baada ya kurejea nchi kwake akitokea Tehran, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alisisitiza haja ya kuondoka askari wa Marekani huko mashariki mwa Furati (Euphrates) nchini Syria haraka iwezekanavyo na kusema kuwa: "Udharura wa kuondoka kwa askari wa Marekani katika eneo hilo la Syria ni moja kati ya matunda ya mkutano wa Tehran. Kwa sababu Marekani inayafadhili na kuyaimarisha kifedha na kijeshi makundi ya kigaidi mashariki mwa Furati (Euphrates) nchini Syria."

Mkutano wa viongozi wa nchi zinazodhamini mchakato wa Astana 

Jeshi la Marekani mbali na kukalia kwa mabavu baadhi ya ardhi za Syria, pia linaiba mafuta ya nchi hiyo na kuyasaidia makundi ya kigaidi kwa fedha na silaha. Ni wazi kwamba, suala hili lina madhara kwa serikali na watu wa Syria, na litazidisha matatizo ya nchi huru na mataifa ya eneo hilo katika siku zijazo. Wakati huo huo, uzoefu umeonyesha kwamba muungano wowote na Marekani na washirika wake hatimaye utazigharimu nchi ambazo zimeipa Washington mkono wa urafiki. Kuhusiana na hilo, Jumanne usiku ulifanyika mkutano wa saba wa nchi wadhamini wa Mchakato wa Astana mjini Tehran ambao ulihudhuriwa na marais wa Iran, Russia na Uturuki. Miongoni mwa sehemu muhimu za mkutano huo wa Tehran ni kukutana maraisi hao na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na jinsi walivyoyapa mazingatio mapendekezo yake. Katika kikao chake na Marais wa Iran, Russia na Uturuki, Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo suala la kulindwa ardhi yote ya Syria na kusema: Shambulio lolote la kijeshi katika eneo la kaskazini mwa Syria litazidhuru Uturuki, Syria na eneo zima na Asia Magharibi na kuwanufaisha magaidi. Akiashiria chuki ya Rais wa Uturuki dhidi ya makundi ya kigaidi amesema: "Ugaidi lazima upigwe vita, lakini shambulio la kijeshi nchini Syria litawanufaisha magaidi. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa magaidi hawaishii katika kundi makhsusi. 

Katika siku za hivi karibuni maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Uturuki akiwemo rais wa nchi hiyo walizungumza kuhusu maandalizi ya shambulio jingine la kijeshi dhidi ya Syria. Ni dhahiri kwamba kudhoofika kwa serikali halali ya Bashar al-Assad nchini Syria kupitia operesheni za kijeshi kutakuwa na madhara kwa nchi za eneo la Magharibi mwa Asia na kuzinufaisha ya nchi za kigeni na hata harakati za wanamgambo wenye mfungamano na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi. Kwa maneno mengine ni kuwa, iwapo Uturuki itafanya operesheni za kijeshi nchini Syria, makundi ya wanamgambo wenye mfungamano na nchi za Magharibi na harakati za kigaidi za kitakfiri ndizo zitakazofaidika na mashambulizi hayo. Kwa hakika kudhoofika kwa serikali ya Bashar al-Assad kutapelekea kuimarika kwa harakati za kigaidi ambazo serikali ya Uturuki imeikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Syria kwa kisingizio cha kukabiliana nazo. Hapo awali, viongozi wengi wa vyama vya upinzani dhidi ya serikali ya Erdogan walikuwa wametoa tahadhari kuhusiana na suala hili. Hata hivyo inaonekana kuwa serikali ya Ankara haijazingatia mapendekezo haya. Taha Ak Yul, mmoja wa wachambuzi na wanasheria mashuhuri wa Uturuki, anazungumzia operesheni ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mwa Syria na kusema: "Upinzani wa nchi kadhaa zenye nguvu dhidi ya operesheni hiyo ni kielelezo cha upweke na kutengwa  Uturuki katika sera ya kigeni ya serikali ya Recep Tayyip Erdogan." 

Rais Bashar al Assad wa Syria 

Kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, jeshi la Uturuki linakalia kwa mabavu maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Syria kwa miaka kadhaa. Uvamizi huo wa Uturuki umelaaniwa na serikali na watu wa Syria na vilevile jamii ya kimataifa. 

Kwa vyovyote vile, kwa mujibu wa matamshi ya juzi ya Rais wa Uturuki, inaonekana kwamba baada ya mkutano wa Tehran, serikali ya Ankara haina nia ya kuidhoofisha serikali halali ya Bashar al-Assad nchini Syria. Suala hili linatambuliwa kuwa ni sehemu ya matunda na mafanikio ya mkutano wa Tehran. 

Tags