Iraq: Kikao kijacho cha Iran na Saudia mjini Baghdad kitafanyika hadharani
(last modified Sun, 24 Jul 2022 02:23:37 GMT )
Jul 24, 2022 02:23 UTC
  • Iraq: Kikao kijacho cha Iran na Saudia mjini Baghdad kitafanyika hadharani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema, kikao kijacho cha Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Baghdad kitakuwa cha mazungumzo ya wazi kutokana na ombi lililotolewa na mrithi wa ufalme wa Saudia.

Januari 3, 2016 Saudi Arabia iliamua kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran kwa kisingizio cha baadhi ya watu kushambulia ubalozi wake mjini Tehran na ubalozi wake mdogo mjini Mashhad.

Hadi sasa zimeshafanyika duru tano za mazungumzo kati ya Iran na Saudia mjini Baghdad, Iraq kwa madhumuni ya kuufufua tena uhusiano baina ya nchi hizi mbili.

Katika duru ya tano ya mazungumzo kati ya wawakilishi waandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia mjini Baghdad, ulijitokeza mwanga mkubwa zaidi wa matumaini ya kuanzishwa tena uhusiano baina ya nchi mbili.

Fuad Hussein

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein ametangaza kuwa, mazungumzo yajayo kati ya Tehran na Riyadh mjini Baghdad yatafanyika kwa njia ya wazi na katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbili.

Fuad Hussein ameongeza kuwa, hadi sasa vimefanyika vikao vitano kuhusiana na masuala ya usalama; na hivi sasa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia ameitaka Iraq iitishe kikao kati ya waziri wa mambo ya nje wa Saudia na mwenzake wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alieleza hivi karibuni kuhusu mazungumzo ya Iran na Saudia kwamba Riyadh imetangaza kuwa iko tayari kufanya mazungumzo ya kisiasa na ya wazi na Tehran.

Aidha, Amir-Abdollahian amesema, mabalozi wa Muungano wa Falme za Kiarabu na Kuwait karibuni hivi watarudi mjini Tehran.../

Tags