Kuendelea mkwamo wa kisiasa nchini Lebanon
Licha ya kupita zaidi ya miezi miwili tangu kuteuliwa Najib Mikati kuwa Waziri Mkuu wa Lebanon, lakini hadi sasa nchi hiyo ingali inakabiliwa na mkwamo wa kisiasa hususan kuhusiana na uundwaji wa serikali.
Mkwamo wa kisiasa nchini Lebanon hauhusiana na kipindi cha miezi mitatu ya hivi karibuni tu, bali ni miaka mitatu sasa ambapo nchi hiyo inakabiliwa na hali hiyo. Ilikuwa Oktoba 2019 wakati kulipoibuka maandamano makubwa yaliyompelekea Waziri Mkuu Sa'ad al-Hariri kujiuzulu ili kwa njia hiyo akwepe kubebeshwa mzigo wa lawama hasa kuhusiana na changamoto kubwa ya kiuchumi. Aidha Saad Hariri al-Hariri alifanya hivyo ili kuanda mazingira pia ya kushadiidisha mpasuko wa ndani nchini Lebanon. Kabla ya kujiuzulu la-Hariri, Lebanon ilikuwa ikikabiliwa na matatizo machache ikilinganishwa na kipindi cha baada ya kujiuzulu kwake.
Baada ya kujiuzulu Saad al-Hariri, serikali ya Hassan Diab ikachukua nafasi hiyo, hata hivyo nayo ililazimika kujiuzulu kutokkana na changamoto mtawalia sambamba na upinzani iliokabiliwa nao hususan kutoka kwa makundi yanayomuunga mkono Saad al-Hariri. Pigo la mwisho dhidii ya serikali ya Hassan Diab lilikuwa mlipuko wa Agosti nne katika bandari ya Beirut ambao ulisababisha zaidi ya watu 6,000 kuuawa na kujeruhiwa. Kuanzia hapo Lebanon ikaangia katika kipindi cha serikali za mpito. Serikali ya Hassan Diab iliendelea kuongoza kama serikali ya muda hadi Oktoba 2021 wakati Najib Mikati alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya.
Najib Mikati alifanikiwa kuitisha uchaguzi wa Bunge mwezi Mei mwaka huu na baada ya hapo akateuliwa na kutangazwa kuwa Waziri Mkuu. Hata hivyo, licha ya kupita miezi kadhaa tangu achukue wadhifa huo, hadi sasa hajafanikiwa kuunda serikali,
Anga ya siasa nchini Lebanon iko kwa namna ambayo, kidhahiri mirengo ya kisiasa iliyoko karibu na mrengo wa Machi 14 haina hamu ya kuundwa serikali mpya kwani inasubiri kipindi cha uongozi cha Rais Michel Aoun kimalizike ili serikali mpya iunde kukiwa na Rais mpya. Kipindi cha uongozi cha Michel Aoun kinamalizika Oktoba mwaka huu (2022).
Inaonekana kuwa, tatizo kubwa katika mchakato wa kuunda serikali nchini Lebanon ni hisa na ugavi wa wizara kwa mirengo mbalimbali ya kisiasa ya nchi hiyo. Wizara kama ya nishati na Mambo ya Ndani ni miongoni mwa wizara zilizozusha mizozo na hitilafu ambapo kila mrengo unataka upatiwe wizara hizo. Mkwamo wa sasa wa kuunda serikali mpya nchini Lebanon unashuhudiwa katika hali ambayo, kabla ya hapo, Saad al-Hariri alikabiliwa na changamoto kama hii ambapo alishindwa kuunda serikali kwa muda wa takribani mwaka mmoja. Kutokana na kuendelea mkwamo wa kisiasa na hilo kushuhudiwa kila mara katika uundaji serikali inaonekana kuwa, mpasuko wa kisiasa nchini Lebanon unachukua wigo mpana zaidi.
Kwa kuzingatia hali hiyo tunaweza kusema kuwa, kuna giza mbele kuhusiana na uteuzi wa rais mpya. Kwa mujibu wa katiba ya Lebanon na ada inayotawala nchini humo, kikawaida Rais anapaswa kuchaguliwa na Bunge mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi cha Rais aliyeko madarakani ili kwa njia hiyo pasiwepo na ombwe la cheo cha Rais na kulazimika kuweko kipindi cha mpito. Mara iliyopita ilipita takribani miezi 30 mpaka kuja kuchaguliwa Michel Aoun kuwa Rais.
Nukta nyingine ni hii kwamba, licha ya Lebanon kuwa nchi ndogo kimasafa, lakini ni nchi muhimu katika eneo la Asia Magharibi. Ni kutokana na hali hiyo ndio maana kiwango cha uingialiaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Lebanon kiko juu mno. Tawala za Marekani na Saudi Arabia ni miongoni mwa mataifa ambayo yamekuwa yakiingilia suala la kuundwa serikali nchini Lebanon. Katika hali ambayo, Lebanon inakabiliwa na hali mbaya kabisa ya kiuchumi, Marekani haiko tayari kusitisha vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Hii ni kutokana na kuwa inaamini kuwa, eti vikwazo ni wenzo dhidi ya Hizbullah ambao unaweza kupunguza nguvu na ushawishi wa harakati hiyo katika uundaji wa serikali mpya nchini Lebanon. Ali Damush, Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon anasema: donda la saratani ambalo leo limewazingira Walebanon na kushadidisha mgogoro wa nchi hiyo ni Marekani ambayo imekuwa ikizuia hata misaada kuwafikia Walebanon.