Saudia yatishia kuikatia UN ufadhili kwa kuiweka kwenye orodha nyeusi
Saudi Arabia imetishia kukata misaada na ufadhili wake kwa Umoja wa Mataifa, siku chache baada ya Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa umoja huo kuuweka muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na nchi hiyo dhidi ya Yemen kwenye orodha yake nyeusi.
Duru za habari zimearifu kuwa, ofisi ya Ban Ki-moon imekuwa ikipokea simu kutoka mawaziri wa mambo ya nje wa nchi sita wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kuishinikiza UN iuondoe utawala wa Aal-Saud katika orodha hiyo. Vyanzo vya habari vinasema kuwa, Saudia inatumia kila njia yakiwemo mashinikizo na vitisho kuutaka Umoja wa Mataifa uuodoea utawala huo wa kifalme katika orodha hiyo nyeusi. Mbali na kutumia Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika kuishinikiza UN, utawala wa Riyadh umetishia kuwaagiza wanazuoni wake watoe fatwa ya kusema kuwa sera za Umoja wa Mataifa zinapingana na Uislamu. Jumatatu iliyopita, Umoja wa Mataifa uliondoa jina la Saudi Arabia kwenye orodha hiyo kwa muda, ukidai kuwa unaangalia upya kadhia hiyo. Siku chache zilizopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kupitia ripoti maalumu alitangaza msimamo wa kuuweka muungano vamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen katika orodha yake nyeusi, ambapo mbali na kukosoa vikali mashambulio ya muungano huo unaoongozwa na utawala wa Aal-Saudi dhidi ya Yemen, alisema muungano huo ndio unaobeba dhima ya mauaji ya halaiki ya watoto wa Yemen. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa kutokana na kuongezeka na kuenea mapigano nchini Yemen, ukatili dhidi ya watoto wa nchi hiyo umeongezeka kwa kiwago cha kutisha. Maelfu ya wananchi wa Yemen wakiwemo mamia ya wanawake na watoto wadogo wameshauawa na wengine wengi kujeruhiwa huku asilimia 80 ya miundombinu ya Yemen ikiwa imeharibiwa kikamilifu, tokea muungano huo uanzishe hujuma dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu Machi mwaka jana 2015.