Afisa wa Hamas: Ukingo wa Magharibi umekuwa kitovu cha muqawama
Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Jenin vimekuwa hifadhi na nguzo ya muqawama.
Vijana na makundi ya muqawama ya Palestina yametangaza mara kadhaa kuwa, mapambano baina yao na utawala haramu wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu yako wazi kote Palestina na ni mapambano ya pande zote. Ameongeza kuwa dhulma na jinai za Israel haziwezi kusitisha azma ya wananchi wa Palestina na kuwazuia kuendelea mbele na muqawama kama chaguo lao pekee la kujikomboa katika makucha ya utawala huo.
Televisheni ya Almasirah ya Yemen imeripoti kuwa, Ismail Ridhwan mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu wa Hamas ameeleza kuwa, adui Mzayuni anakabiliwa na changamoto kubwa na hawezi kuushambulia kiurahisi mji wa Jenin. Amesisitiza kuwa, muqawama katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umepiga hatua kwa kumiliki silaha sambamba na kutekelezwa operesheni za kutumia silaha baridi na kuwadhibiti Wazayuni.
Ismail Ridhwan amesema mapambano katika Ukingo wa Magharibi sasa yamewanyima usingizi viongozi wa utawala wa Kizayuni kuliko wakati mwingine wowote.