Israel yawakataza Wapalestina kutembeleana mwezi wa Ramadhan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8833-israel_yawakataza_wapalestina_kutembeleana_mwezi_wa_ramadhan
Utawala wa Kizayuni wa Israel umewapiga marufuku Wapalestina kutembeleana na kufanya ziara katika maeneo matakatifu ya ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu, katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, kufuatia shambulizi dhidi ya Tel Aviv.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 09, 2016 09:25 UTC
  • Israel yawakataza Wapalestina kutembeleana mwezi wa Ramadhan

Utawala wa Kizayuni wa Israel umewapiga marufuku Wapalestina kutembeleana na kufanya ziara katika maeneo matakatifu ya ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu, katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, kufuatia shambulizi dhidi ya Tel Aviv.

Taarifa iliyotolewa leo Alkhamisi na utawala huo haramu imesema kuwa, ni marufuku kwa Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwatembelea ndugu na jamaa zao katika Ukanda wa Gaza. Tayari utawala haramu wa Israel umebatilisha vibali 83,000 vya kuwaruhusu Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi kuutembelea Ukanda wa Gaza ulioko chini ya mzingiro wa kibaguzi. Aidha kwa mujibu wa taarifa ya utawala ghasibu wa Israel, Wapalestina hawaruhusiwi kuzuru maeneo matakatifu kama Haram al-Sharif, iliyoko katika mji mtukufu wa Quds. Wakati huo huo, Benjami Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametahadharisha kuwa maafisa wa usalama wa utawala huo katili watashadidisha operesheni zao wakati huu, kufuatia shambulizi la Tel Aviv la jana usiku, ambapo Wazayuni wanne waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Hii ni katika hali ambayo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema operesheni ya shambulizi lililotekelezwa dhidi ya Wazayuni ni matokeo ya jinai zilizoshtadi za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.