Hamas: Kuendelea kuhujumiwa al-Aqsa 'kutalipua' Asia Magharibi
(last modified Wed, 28 Sep 2022 08:12:27 GMT )
Sep 28, 2022 08:12 UTC
  • Hamas: Kuendelea kuhujumiwa al-Aqsa 'kutalipua' Asia Magharibi

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amelaani vikali hujuma na uvamizi unaoendelea wa wanajeshi wa Kizayuni na walowezi wa Kiyahudi dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqsa katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.

Hazem Qassem ameashiria matukio yanayojiri sasa huko Quds na kubainisha kuwa, hatua ya Wazayuni ya kuuvamia msikiti huo ni kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu, na vitendo hivyo yumkini vikaripua ghadhabu za umma wa Kiislamu zisizoweza kudhibitika.

Amesema hatua za namna hii za kichokozi zinachukuliwa kwa lengo la kuumiza hisia za Waislamu wote kote duniani, na kwamba Wazayuni watabeba dhima ya matokeo mabaya ya chokochoko hizo.

Kabla ya hapo, Dkt. Mahmoud al-Zahar, Mjumbe mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya HAMAS alisema kuwa, utawala haramu wa Israel unatumia vibaya udhaifu ambao umeugubika ulimwengu wa Kiarabu na hivyo kuudhibiti mji wa Beitul-Muqaddas na msikiti mtakatifu wa al-Aqsa.

Hazem Qassem

Aidha Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar sambamba na kulaani hujuma na uvamizi huo imesema kuwa, njama za Wazayuni zilizoratibiwa huko Quds zitapelekea kutokea mlipuko na kuanza tena machafuko.

Tangu juzi Jumatatu walowezi wa Kiyahudi wameshadidisha hujuma na uvamizi wao dhidi ya msikiti wa al-Aqswa kwa kisingizio cha kuanza mwaka mpya wa Kiyahudi.

Wanajeshi wa Israel wamekuwa wakitoa himaya na kusaidia walowezi hao katika hujuma zao sambamba na kukabiliana na vijana wa Kipalestina wanaojitokeza kuuhami na kuulinda msikiti huo mtakatifu, kibla cha kwanza cha Waislamu.

Tags