UN yaikosoa Israel kuwakataza Wapalestina kuingia katika ardhi zao
Umoja wa Mataifa umeukosoa utawala haramu wa Israel kwa kuwazuia Wapalestina kuingia na kutembea katika ardhi zao unazozikalia kwa mabavu.
Zeid Ra'ad al-Hussein, Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema kutengua vibali vya Wapalestina kutembelea ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu ni kukiuka sheria ya kimataifa iliyopiga marufuku kutoa adhabu kwa kaumu au kundi la watu wakati kosa au jinai imefanywa na watu fulani miongoni mwao. Taarifa iliyotolewa Alkhamisi na utawala haramu wa Israel ilisema kuwa, ni marufuku kwa Wapalestina kuingia katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu. Utawala huo haramu umebatilisha vibali 83,000 vya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi na 200 vya wenzao wa Ukanda wa Gaza ulioko chini ya mzingiro wa kibaguzi, kuingia katika ardhi zao zinazikaliwa kwa mabavu. Utawala huo wa Kizayuni umewapiga marufuku Wapalestina kutembeleana na kufanya ziara katika maeneo matakatifu ya ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu, kufuatia hujuma dhidi ya Tel Aviv Alkhamisi usiku, ambapo Wazayuni wanne waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Haya yanajiri huku msemaji wa jeshi la utawala huo ghasibu wa Israel akidai kuwa, marufuku hiyo dhidi ya Wapalestina itamalizika Jumapli usiku.