Iraq katika mchakato wa kuvuka mkwamo wa kisiasa wa mwaka mmoja
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i89326-iraq_katika_mchakato_wa_kuvuka_mkwamo_wa_kisiasa_wa_mwaka_mmoja
Hatimaye bunge la Iraq limemchagua rais mpya wa nchi hiyo Abdul Latif Rashid ambapo rais huyo pia katika hatua yake ya awali amemteua Mohammed Shia al-Sudani kuwa Waziri Mkuu na kumpatia jukumu la kuunda serikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 16, 2022 02:30 UTC
  • Iraq katika mchakato wa kuvuka mkwamo wa kisiasa wa mwaka mmoja

Hatimaye bunge la Iraq limemchagua rais mpya wa nchi hiyo Abdul Latif Rashid ambapo rais huyo pia katika hatua yake ya awali amemteua Mohammed Shia al-Sudani kuwa Waziri Mkuu na kumpatia jukumu la kuunda serikali.

Uchaguzi wa bunge nchini Iraq ulifanyika mwezi Oktoba mwaka jana. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni Mohammed al Halbousi pekee ambaye bunge la Iraq lilimpigia mara mbili kura ya kuwa na imani naye na hivyo kushikilia nafasi ya spika wa Bunge. Kura hiyo mara ya kwanza ilifanyika kwa kuhudhuriwa na wabunge wa mrengo wa Sadr, na mara ya pili pia baada ya kujiuzulu bungeni wabunge hao. Mwaka uliopita nyadhifa mbili hizo za rais na waziri mkuu zilikuwa zikishikiliwa na Barhum Saleh na Mustafa al Kadhimi; na wakati huo wabunge walishindwa kuwaarifisha rais na waziri mkuu mpya wa Iraq.  

Baada ya kupita mwaka mmoja na siku tatu tangu uchaguzi wa bunge ufanyike huko Iraq na licha ya kuwepo mivutano ya muda mrefu kati ya vyama viwili vikuu vya Kikurdi hatimaye kikao cha kumchagua rais mpya wa Iraq kilifanyika Alhamisi Oktoba 13. Abdul Latif Rashid alipata kura 162 na hivyo kufanikiwa kumuondoa katika duru ya mchuano Barhum Saleh aliyepata kura 99 baada ya kuhesabiwa kura zote zilizopigwa katika duru ya pili ya upigaji kura bungeni; na hivyo akawa rais mpya rasmi wa Iraq. Baada ya hapo, Rais Abdul Latif Rashid pia alimpatia jukumu Mohammed Shia al-Sudani la kuunda serikali.  

Abdul Latif Rashid, Rais mpya wa Iraq 

Kuainishwa katika ngazi ya awali Abdul Latif Rashid kuwa rais mpya wa Iraq kumejiri baada ya kuwekwa kando hitilafu kubwa kati ya vyama viwili vikuu vya Wakurdi yaani chama cha Kidemokrasia na kile cha Umoja wa Wazalendo wa Kurdistan. Huko Iraq, rais wa nchi kwa kawaida huchaguliwa miongoni mwa shakhsia wa Kikurdi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita vyama hivyo viwili vikubwa vya Wakurdi viilikuwa vikihitilafiana pakubwa kuhusu suala la rais mpya. Chama cha Kidemokrasia ambacho kilikuwa kimepata viti vya uwakilishi bungeni mara mbili zaidi ya vile vya chama cha Umoja wa Wazalendo wa Kurdistan kiliamini kwamba kinapasa kumuarifisha rais huku chama cha Umoja wa Wazalendo wa Kurdistan kikiamini kuwa kilikuwa na haki ya kumuarifisha rais wa nchi kama ilivyokuwa katika duru zilizopita. 

Kufuatia kutangazwa  Abdul Latif Rashid kuwa rais mpya wa Iraq, Masoud Barzani Mkuu wa chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan alifanya mazungumzo ya simu na Abdul Latif Rashid na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuwa rais wa Iraq. Barzani aidha alisisitiza kumuunga mkono rais huyo mpya wa Iraq na kueleza matarajio yake kuwa, mchakato wa kisiasa wa Iraq utaelekea katika marhala chanya. Mazungumzo ya simu kati ya Masoud barzani na Abdul Latif Rashid waliyofanya muda mfupi baada ya kuchukua wadhifa huo yanaonyesha kuwa mirengo miwili mikuu ya Wakurdi angalau imeweka kando hitilafu zao katika suala la kumuarifisha rais mpya. 

Masoud Barzani 

Hatua ya Abdul Latif Rashid ya kumpatia jukumu la kuunda serikali Mohammed Shia al-Sudani pia inadhihirisha namna Muungano wa Kishia  wa Coordination Framework Alliance ulivyoasisi mrengo mkubwa zaidi ndani ya bunge la Iraq. Ni wazi kuwa, ingeshindikana pia kumuarifisha rais mpya wa Iraq kama mrengo wa Kishia usingekuwa na utengamano. Kwa msingi huo, inaonekana kuwa mwisho wa uongozi wa Mustafa al Kadhimi waziri mkuu wa muda wa Iraq pia umekaribia na Shia al- Sudani atafanikiwa kuunda serikali mpya nchini. Tukio  hilo licha ya kuhesabiwa kuwa pigo kubwa kwa mrengo wa Sadr ambao mwaka mmoja uliopita ulikwamisha kwa vizuizi mbalimbali kuarifishwa waziri mkuu na kuundwa serikali huko Iraq pia linaonyesha kupatikana umoja kati ya makundi ya kisiasa ya Iraq kwa ajili ya kuvuka mkwamo wa kisiasa ulioigubika nchi hiyo kwa muda mrefu. Ndio maana Masoud Barzani Mkuu wa chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan juzi usiku akawasiliana kwa simu na Muhammad Shia al Sudani Waziri Mkuu aliyepewa jukumu la kuunda serikali mpya huko Iraq na kujadiliana naye kuhusu kadhia hiyo.