OIC: Russia ni mshirika wetu muhimu sana
-
Hussain Ibrahim Taha
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ameitaja Russia kuwa ni mshirika muhimu sana wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Hussain Ibrahim Taha amesisitiza umuhimu wa kuwa na urafiki na Russia na wakati huo huo akatilia mkazo udharura wa kustawisha uhusiano na nchi hiyo kama nchi mtazamaji ndani ya OIC.
Hussain Ibrahim ambaye juzi Jumapili alielekea Moscow, Russia, akiuongoza ujumbe wa OIC ameeleza kuwa: "Dunia imeanza kuelewa kile kinachojiri sasa ulimwenguni na kwa hiyo ni wakati mwafaka sasa wa kueleza wazi urafiki wetu na Russia na umuhimu wa kuendeleza mahusiano kati yetu."
Ziara ya karibuni ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Moscow imefanyika katika fremu ya uhusiano wa kihistoria na wa kimkakati kati ya Russia na Ulimwengu wa Kiislamu na kwa lengo la kufanya mashauriano kuhusu masuala ya amani na usalama wa dunia.
Katibu Mkuu wa OIC amekuwa pia na mazungumzo na Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa nchi hiyo. Pande hizo zimejadili masuala ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali kati ya OIC na Moscow.